Wednesday, August 5, 2009

JAMBAZI LAUAWA NA WANANCHI KWA KUCHOMWA MOTO

MTU mmoja anayetuhumiwa kuwa jambazi, ameuawa kwa kupigwa na baadaye kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali wa mji mdogo wa Mlowo, wilayani Mbozi.

Tukio hilo lilitokea jana saa 11;00 alfajiri baada ya jambazi huyo akiwa na mwenzake mmoja aliyefanikiwa kukimbia, kukurupushwa eneo la darajani na sungusungu waliokuwa doria.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wakazi wa mji huo walisema kuwa Sungusungu hao wakiwa doria waliwakuta watuhumiwa hao wawili wakiwa na nondo pamoja na mapanga, hali iliyoonyesha kuwa walikuwa wakienda kufanya uharifu.

Walisema mara baada ya kukurupushwa, mmoja alifanikiwa kukimbia na kumuacha mwenzake ambaye alipata kipigo kikali hadi kupoteza fahamu ambapo waliwaacha baadhi ya sungusungu wakimlinda na wengine kuendelea kumtafuta aliyekimbia.

“Mmoja wa watuhumiwa hao alifanikiwa kukimbia na ilidaiwa kuwa amejificha katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Altimalta iliyopo Mlowo.Viongozi wa serikali ya mtaa walilazimika kuwaomba wananchi waliokuwa wamejitokeza kuondoka eneo hilo lakini ilishindikana” walisema.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya raia wema walikimbilia kituo kidogo cha polisi Mlowo na kutoa taarifa ambapo walifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kuwataka wananchi kuondoka lakini waliendelea kukaidi amri hali iliyowalazimisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatanya.

Polisi walifanikiwa kuwakamata Paulo Dulle na mhudumu wa nyumba hiyo ya wageni,aitwaye Taida ambapo wananchi wakiwa mikono mitupu waliandamana hadi kituoni hapo na kuwataka polisi wamuachie Dulle ili wamuue pia.

Naye Meneja wa nyumba hiyo ya kulala wageni Altimalta, Furaha Mgalla alisema Julai 1,mwaka huu, aliwapokea wapangaji watatu aliowataja kuwa ni Ezekia Mbope, Paulo Dulle ambaye ni mpiga ramli, mkazi wa Tunduma na Salum.

Mgalla aliongeza kuwa jana saa 5:00 usiku, kulitokea ugomvi wa kimapenzi kati ya mhudumu wake aliyemtaja kwa jina moja la Taida na mpangaji Dulle, hali iliyopelekea aingilie kati ili kuleta suluhu.

“Baada ya kuwafuata mhudumu wangu Taida alidai kuwa Dulle alitaka kumkaba na amempora shilingi 80,000, ambapo nilipomuuliza Dulle hakutaka kuongea na badala yake alitoka nje.Mwenzake Salum alipoelezwa kilichojiri alianza kumpiga Dulle”alisema Mgalla.

Aliongeza kuwa kelele za ugomvi huo ziliwafikia Sungusungu, ambao walifika eneo hilo na kuwakamata Taida pamoja na Salum na kuwapeleka kituo kidogo cha polisi Mlowo, lakini Dulle alikataa kukamatwa.

Mgalla alisema ndipo Sungusungu hao walipotoka hapo na kuendelea na doria ambapo, waliwakuta vijana hao wawili eneo la darajani wakijianda kwenda kufanya uharifu na kuwazingira ambapo mmoja alifanikiwa kukimbia.

Taarifa zaidi zilizopatikana kwa watu walishuhudia tukio hilo, walisema mara baada ya kumuacha majeruhi huyo na kuanza kumfuata mwenzake aliyekuwa amekimbia, nyuma baadhi ya Sungusungu waliokuwa wameachwa na majeruhi huyo waliamua kutafuta majani na kuanza kumchoma moto mtuhumiwa.

Zilidai kuwa ndipo mtuhumiwa huyo alipokurupuka huku akipiga kelele, na kwenda kujitumbukiza katika mto ulio karibu na eneo hilo ili kuuzima moto uliokuwa ukiwaka mwilini mwake, na kelele hizo zilivuta kundi la watu waliofika na kumpiga na kisha kumchoma moto.

Imeelezwa kuwa Sungusungu hao walioondoka na kwenda moja kwa moja katika nyumba ya kulala wageni Altimalta kwani inadaiwa kuwa walikuwa na mashaka na kundi la watu hao watatu waliokuwa wamepanga hapo kuwa ni majambazi.

Hivyo walihisi kuwa mtuhumiwa aliyekimbia ni mmoja wa wapangaji watatu waliokuwa wakiwatilia mashaka, ambap walipofika waliizingira nyumba hiyo ya wageni ili kuhakikisha kuwa hakuna anayefanikiwa kutoroka.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Advocate Nyombi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la mauaji lakini alisema marehemu hajatambulika jina na kwamba wanawashikilia watu wawili kwa upelelezi zaidi.

Nyombi aliongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya wilaya Vwawa.

UVCCM YATOA UFAFANUZI KUHUSU RIDHWANI KIKWETE

UONGOZI wa jumuia ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilaya ya Kyela, umepinga uzushi unaonezwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UVCCM Taifa, Ridhwan Kikwete, alizuiwa kushiriki harambee wilayani humo.

Imeelezwa kuwa UVCCM wilaya hiyo walimuomba Kikwete kuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo iliyofanyika Julai 31,mwaka huu kwa kuwa ni kiongozi wa kitaifa wa jumuia hiyo na si vinginevyo.

Katibu wa UVCCM wilaya ya Kyela, George Silindu, aliyasema hayo wilayani humo kufuatia habari moja iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku (jina linahifadhiwa) kuwa Kikwete aliingia mitini baada ya kuzuiwa na kundi moja la kisiasa wilayani humo.

Silindu alisema walianza kufanya mawasiliano na Kikwete kwa njia yam domo tangu mwaka 2008, ambapo mawasiliano rasmi ikiwa ni kumuandikia barua kupitia Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa yalianza mwezi Februali mwaka huu.

“Tulimualika awe mgeni rasmi katika harambee yetu kwa ajili ya kutafuta mtaji wa UVCCM wilaya ya Kyela…Makadirio yetu yalikuwa ni kupata shilingi milioni 155 kwa awamu mbili tofauti” alisema Silindu.

Aliongeza kuwa Julai 31, mwaka huu baada ya kufanya mawasiliano na Mjumbe huyo wa Kamati ya Utekelezaji UVCCM Taifa, waliandaa mapokezi eneo la Busale, ambapo walikaa hadi saa 11:00 jioni bila ya kiongozi huyo kutokea.

Alifafanua kuwa waliamua kurudi ukumbi wa KBC uliopo Kyela mjini, ambako ndiko harambee ilikuwa ifanyike wakiwa wameongozana na viongozi wa UVCCM mkoa wa Mbeya pamoja na wawakilishi wa CCM mkoa ambao waliongozwa na Katibu wa Uchumi na fedha Keneth Ndingo.

Katibu huyo wa UVCCM wilaya alisema iliwabidi kuendesha harambee hiyo kama walivyokuwa wamepanga, lakini walishindwa kutangaza kiwango kilichopatikana kwa kuhofia kuwa Kikwete anaweza kutokea wakato wowote wakiwa ukumbini humo.

Silindu alisema Kamati maalumu ya harambee hiyo leo (jana), ilikuwa inatarajiwa kukutana kwa ajili ya kufanya tathmini nzima ya harambee hiyo na ndio itatangaza kiasi cha fedha kilichopatikana.

Aliongeza kuwa mbali ya kuendesha harambee hiyo, Kikwete pia alikuwa amepangiwa kazi ya kufungua matawi mawili ya UVCCM katika maeneo ya Ipinda na Ngyeke yaliyopo kata ya Matema na baadaye ahutubie mkutano wa hadhara katika kata hiyo.

“Tulimualika Kikwete kwa kuwa ni kiongozi wa kitaifa wa UVCCM,lakini hatukumualika kwa makusudi mengine yoyote kama inavyoenezwa…hivyo siyo sahihi kuwa alizuiwa kuja Kyela na kundi moja la kisiasa wilayani humu” alisema Silindu.

Alifafanua kuwa Kikwete asingekuwa kiongozi wa jumuia hiyo ngazi ya kitaifa, ndio ilipaswa watu wahoji kuwa ameenda wilayani humo kama nani lakini itambulike kuwa ni kiongozi wa kitaifa na ndiyo iliyoisukuma jumuia hiyo kumualika.

Silindu alisema kuwa UVCCM wilaya hiyo haiwezi kushtushwa na Kikwete kutohudhuria harambee, kwani naye ni binadamu kama walivyo wengine hivyo anaweza kupata udhuru uliopelekea ashindwe kufika wilayani Kyela.

Alibainisha kuwa wapo viongozi wengine waliowatumia kadi za mwaliko wakiwemo kutoka Dar es Salaam lakini walishindwa kufika, ila walituma michango yao waliyoahidi hivyo kutofika kwa Kikwete kusiwe nongwa.

“Kwa mtu mwenye shaka yoyote juu ysa ujio wa Kikwete ni vyema awasiliane na Mwenyekiti wa UVCCM wilayani hapa, Dk.Hunter Mwakifuna ama mimi ili tumpe ufafanuzi lakini siyo kuzusha mambo ambayo hayapo” alisema Silindu kwa msisitizo.

HALMASHAURI WILAYA YA KYELA YASHINDWA KUTUMIA SH.MILIONI 700

MKURUGENZI wa halmashauri ya wilaya Kyela, Harold Senyagwa, amefanya ukaguzi wa ghafla na kubaini jumla ya shilingi 738,317,808 zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2008/09, hazijatumika.

Kufuatia hatua hiyo, ameunda Timu ya Ukaguzi ya watu watatu ili kufanya uchunguzi zaidi kujua sababu zilizopelekea kiasi hicho cha fedha kukaa bila kutumika hadi mwaka mwingine wa fedha unaanza.

Akithibitisha hilo kwa mwandishi wa habari hizi jana ofisini kwake, Senyagwa alisema kuwa alifanya ukaguzi huo Juni 15,mwaka huu wakati zimebakia siku kumi na tano kabla ya mwaka wa fedha kumalizika ili kujua kiasi cha fedha kilichotumika.

Mkurugenzi huyo Mtendaji alizitaja baadhi ya idara zilizobakiza fedha na kuwa ni Afya kwa upande wa ‘Busket fund’ sh.milioni 40.4, Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) sh.milioni 45.4, Ukimwi sh.140.8 na Kilimo na Mifugo sh.milioni 400.

“Lakini tumebaini pia kuna fedha nyingine ziliingia Juni 12,mwaka huu ambazo ni za MMAM sh.24.4 na RWSSP shilingi milioni 41.2.Hivyo ilikuwa ni vigumu kwa fedha hizo kutumika bila kufuata utaratibu uliowekwa na serikali” alisema Senyagwa.

Aliongeza kuwa aliwaandikia barua wakuu wa Idara ambao hawakutumia fedha zao walizokuwa wametengewa ambapo baadhi aliridhika na maelezo waliyoyatoa na wengine hakuridhika na maelezo yao.

Alizitaja idara alizoridhika na maelezo waliyotoa kuwa ni za MMAM, RWSSP na Kilimo ambao nao walipata fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni 70 mwezi Machi, mwaka huu kwa ajili ya kuendeleza Kilimo.

Senyagwa alisema mbali ya kuunda timu ya kuchunguza sababu iliyopelekea fedha hizo zisitumike pia tayari ametoa taarifa hiyo kwa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya halmashauri hiyo juu ya suala hilo.

“Baada ya timu hii ya watu watatu kumaliza kufanya uchunguzi wao na kuniletea walichobaini itajulikana ni hatua zipi zichukuliwe” alisema Senyagwa.

Aliongeza kuwa pia hiyo ya Kamati ya Fedha imependekeza kuwa fedha hizo zaidi ya shilingi milioni 700 zifanyiwe Mpango mkakati wa kuhakikisha zinatumika ili zisiingiliane na bajeti ya mwaka huu wa fedha 2009/10.

Mkurugenzi alisema hivi sasa utekelezaji wake unaendelea lakini amewataka Wakuu wa idara ndani ya halmashauri ya Kyela, kuanza kuoredhesha na kukamilisha mahitaji mapema yakiwemo mambo ya tenda (zabuni).Senyagwa alisema:

”Kwa kufanya hivi itapelekea tusiwe na mambo kama haya ya kubakisha fedha hadi mwaka wa fedha unakwisha kwa miaka ijayo…lakini ikumbukwe kuwa mimi Mkurugenzi ndiye niliyeibua na kubaini kiasi hiki cha fedha kubaki”.

WAGOMEA KULIPWA FIDIA KIDUCHU KUPISHA UJENZI WA SOKO JIPYA LA MWANJELWA

WAMILIKI 30 wa nyumba zinazotaka kubomolewa kata ya Ruanda, ili kupisha ujenzi wa soko jipya la kisasa la Mwanjelwa, wamepinga kiwango kidogo cha fidia wanachotaka kulipwa na halmashauri ya jiji la Mbeya.

Imeelezwa kuwa halmashauri hiyo imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili ya kulipa fidia huku kiwango cha juu cha fidia kikiwa ni sh.milioni 82.3 na cha chini ni sh. milioni 9.

Soko la awali Mwanjelwa lililokuwa na wafanyabiashara zaidi ya 900, liliungua na kuteketea kwa moto Desemba mwaka 2006, na kupelekea hasara ya mamilioni ya shilingi.

Wamesema kuwa wanatarajia kuandika barua kwa Mkurugenzi wa jiji kupinga kiwango wanacjhotaka kulipwa na iwapo watapuuzwa basi watafungua kesi mahakamani kupinga nyumba zao kubomolewa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema kuwa nyumba zao hizo zimekaa kibiashara kwani zipo katika mtaa wa soko ambapo wenzao walio umbali wa mita 50 wamekuwa wakiziuza nyumba zao kati ya shilingi milioni 400 hadi milioni 200.

Vitus Swalo mwenye nyumba namba R/049 alisema kuwa yeye licha ya kumiliki nyumba kubwa ya kibiashara anashangaa kuwa katika uthamini uliofanywa na maofisa wa kitengo cha uthamini cha jiji kilichopo chini ya Edina Mwaigomole, anatakiwa kulipwa fidia y ash.milioni 11 kitu ambacho hawezi kukubaliana nacho.

Swalo alisema wao wanakubali nyumba zao kubomolewa ili kupisha ujenzi wa soko hilo lililotengewa jumla ya shilingi Bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wake, lakini hakubaliana na fidia anayotaka kulipwa kwani hailingani na eneo ilipo nyumba yake.

“Fedha ya fidia tunayotaka kulipwa na halmashauri ya jiji la Mbeya ni ndogo na mbaya zaidi ni kuwa hailingani na hasdhi ya jiji bali ni ile ya halmashauri…hatukatai kupisha ujenzi lakini kiwango hatukubaliani nacho” alisema Swalo.

Naye Keneth Mbewe mwenye nyumba namba R/.004 alisema wanapinga kiwango kidogo walichotengewa kwa ajili ya fidia na wanaiomba serikali kuingilia kati ili haki iweze kutendeka na wapate fidia ya kiwango kinacholingana na eneo hilo la kibiashara zilizopo nyumba zao.

Mbewe alisema kuwa wanataka kumuandikia barua Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Mbeya, Elizabeth Munuo, kupinga kiwango hicho kidogo cha fidia na iwapo ombi lao halitasikilizwa basi wapo tayari kwenda Mahakamani kusimamisha zoezi hilo la ubomoaji wa nyumba zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Soko, zilizopo nyumba hizo, Baraka Mwakyabula, alisema uthaminishaji wa nyumba hizo hauendani na hadhi ya jiji licha ya kwamba wananchi wake wameelezwa kuwa eneo hilo linatakiwa lijengwe soko la kisasa lenye hadhi ya jiji.

Naye Diwani wa kata ya Ruanda, Ephraim Mwaitenda, alipofuatwa alikiri kuwa baadhi ya wananchi wanaomiliki nyumba zinazotakiwa kubomolewa ili kupisha ujenzi wa soko hilo jipya, wamelalamikia kiwango kidogo cha fidia wanachotaka kulipwa.

Mwaitenda alisema lakini fedha hizo wanalipwa kulingana na uthamini uliofanywa na kitengo cha Uthamini cha halmashauri ya jiji la Mbeya, kulingana na matofali yaliyotumika kujenga nyumba husika.

“Baadhi ya nyumba zimejengwa kwa matofali ya saruji, matofali ya kuchoma na nyingine zimejengwa kwa matofali mabichi…kwa mantiki hiyo ni wazi kuwa wale waliojenga kwa matofali ya saruji (Block), watalipwa fidia kubwa zaidi” alisema Mwaitenda.

Aliongeza kuwa amewataka wamiliki hao waliokuwa wanapinga kiwango hicho cha fidia kurudi majumbani mwao, kuchukua karatasi za uhakiki na kisha kuzilinganisha na thamani halisi ya nyumba zao.

Mwaitenda alisema:”Nimewataka baada ya hapo iwapo wataona kuwa hawajaridhika na kiwango cha fidia wanachotaka kulipwa wauone uongozi wa jiji la Mbeya, ili suala lao lipatiwe ufumbuzi”.

Wednesday, July 29, 2009

WALIMU JIJINI MBEYA WAZUSHA TIMBWILI OFISI ZA JIJI NA BAADAYE KWA DC.

KUNDI la Walimu zaidi ya 100 wakiwa na jazba jana walivamia ofisi za Elimu na baadaye ofisi za Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Leonidas Gama, wakilalamikia kucheleweshewa malipo yao bila chochote kulipwa tangu mwaka 2001 hadi 2007.

Kitendo hicho cha walimu kuzingira ofisi za elimu jijini hapa saa 2:00 asubuhi, kilipelekea baadhi ya watendaji kuzikimbia ofisi zao wakihofia kuwa wangeweza kupata kipigo kutoka kwa walimu hao.

Walidai kuwa wamekuwa wakifanywa wapumbavu na wanyonge ambapo wamekuwa wakitakiwa kuwasilisha kumbukumbu zao za madai ambapo mchakato umekuwa ukizidi kurefushwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliofuatilia tukio hilo, walimu hao walisema kuwa waliambiwa waende ofisi hizo kati ya Julai 20 na 24 mwaka huu lakini kila mwalimu aliyefika hapo aliambiwa arudi siku nyingine huku wengine wakitakiwa kuwasilisha vielelezo vya madai yao wakati walikwisha kuviwasilisha awali.

Waandishi walifanikiwa kufika ofisi hizo za Ofisa Elimu wa jiji na kukutana na msongamano wa walimu hao waliokuwa wakidai hawawezi kuondoka ofisini hapo hadi madai yao yafanyiwe kazi.

Wakizungumza wakiwa katika makundi, walisema kuwa malimbikizo hayo ni mishahara, nauli za likizo,marekebisho ya mishahara yao kwa waliopandishwa vyeo huku waliorekebishiwa madaraja hawajawahi kupata mishahara mipya kwa muda wa miaka saba.

Naye Ofisa Elimu wa jiji la Mbeya, Aurelia Lwenza alipfuatwa alisema kuwa hajui lolote kuhusu mchakato mzima wa madai hayo ya walimu kwani mchakato mzima ulikuwa ukifanywa na idara ya utumishi kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Walimu(TSD), ofisi yake haikhusiki na madai hayo.

Aurelia aliongeza kuwa hana taarifa na uvamizi wa walimu hao isipokuwa walipofika alilazimika kumuita Ofisa Utumishi anayeshughulikia madai hayo awaondoe walimu hao kwani ofisi za TSD zipo.

Baadaye ndipo kundi hilo la walimu lilipovamia ofisi za Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Gama ili kuwasilisha malalamiko yao, lakini hawakufanikiwa kumkuta kwani na kuelezwa kuwa yupo safarini jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Ofisa Utumishi wa jiji, Lucy Timba hakuweza kuweka wazi kuhusu madai ya walimu hao na na kwamba haelewi sababu zilizowafanya wakusanyike kwenye ofisi hizo badala ya kuutumia muda huo kufundisha.

Lucy alithibitisha wito wa kuitwa kwa walimu hao uliotolewa na Katibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu jiji la Mbeya,Fredy Lucas ambaye hakuweza kupatikana kwani yupo mkoani Morogoro kikazi.

HOSPITALI YA RUFAA MBEYA WATAKIWA KUTENDA HAKI KATIKA MALIPO YA SAA ZA ZIADA.

UONGOZI wa hospitali ya Rufaa Mbeya, umetakiwa kuwalipa wafanyakazi wake malipo ya saa za ziada kwa kufuata ngazi za mshahara (TGHS), na siyo utaratibu uliopo sasa.

Imeelezwa kuwa uongozi huo umekuwa ukiwaweka maofisa katika makundi mawili, lakini wote wamekuwa wakilipwa saa za ziada kwa kima cha chini cha mshahara, hali ambayo inakuwa haiwatendei haki.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), hospitalini hapo, Ismail Zambi, wakati wa hafla ya kuwapa zawadi wafanyakazi bora wa Sikukuu ya Wafanyakazi duniani(Mei Mosi), mwaka huu, iliyofanyika hospitalini hapo.

Mgeni rasmi katika tukio hilo, alikuwa Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Ayuob Omary.

Wafanyakazi saba walipewa zawadi zao akiwemo mfanyakazi bora wa hospitali hiyo kwa mwaka huu ambaye ni muuguzi mkunga, Regina Sithole, aliyezawadiwa shilingi 300,000.

Zambi alisema utaratibu huo unaofanywa na hospitali ya Rufaa Mbeya siyo sahihi kwani umekuwa unawatambua maofisa wenye elimu ya digrii kitu ambacho siyo sahihi.

"Tumekuwa tunawekwa matabaka mawili tofauti wakati kazi ni zile zile...hivyo ingekuwa vyema wangeweka utaratibu wa kuangalia TGHS kwani Utumishi unatutambua kuwa ni maofisa wakati uongozi wa hospitali unamtambua ofisa kuwa ni yule mwenye digrii" alisema Zambi.

Aliongeza kuwa pia kuna mapungufu mengine yaliyopo hospitalini hapo ikiwemo kutowapandisha vyeo wafanyakazi kwa wakati kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Mwenyekiti huyo wa TUGHE alisema vile vile kumekuwepo na tatizo la kutorekebishwa mishahara kwa wakati kwa wanaopandishwa vyeo, kutolipwa mapunjo ya mishahara kwa wanaopandishwa vyeo na kurekebishiwa mishahara yao.

Zambi alisema:"Tunaupongeza uongozi wa hospitali kwa kudumisha utaratibu huu wa kutoa zawadi kwa watumishi hodari wakati wa sherehe za Mei Mosi kwa kila mwaka...".

Naye Rais wa TUCTA Omary alipongeza hatua hiyo ya kuwapatia zawadi watumishi bora, lakini pia alikumbushia kuhusu umuhimu wa kufanya vikao mahali pa kazi kwa kufuata utaratibu uliopo.

Omary alisema kuwa kwa kupitia vikao hivyo uongozi na wafanyakazi wanaweza kuvitumia kuweka wazi kasoro mbalimbali zinazokuwepo na hivyo kuweza kuzipatia ufumbuzi wake.

"Kwa kuwapa zawadi watumishi wenu bora mnakuwa mnawajengea motisha zaidi ya kuwajibika zaidi" alisema Omary.

Wafanyakazi wengine waliopata zawadi zao za shilingi 150, 0000 kila mmoja ni Dk.Henry Mwakayoka, ofisa wa maabara Hilary Mchuka, ofisa muuguzi kitengo cha wajawazito na Watoto Meta, Mwanjaa Kasigwa na ofisa muuguzi kitengo cha huduma ya afya ya akili, Daina Ifwani.

Pia wamo Muuguzi mkunga wa kitengo cha kuhudumia wanaoishi na virusi vya Ukimwi, Eddah Sanjala na Ally Mbasha kutoka upande wa masijala katika sehemu ya utawala.

Monday, July 27, 2009

SUMATRA KUDHITI DALADALA ZISIZTIKETI KWA ABIRIA JIJINI MBEYA.

MAMLAKA ya Udhibiti Wa Usafiri Nchi kavu na Majini (SUMATRA), kanda ya nyanda za juu kusini, imeazimia kupambana na tatizo sugu la wamiliki wa daladala jijini Mbeya la kutopenda kutoa tiketi kwa abiria.

Imeelezwa kuwa tatizo la utoaji wa tiketi kwa abiria wa daladala jijini Mbeya, limekuwa sugu hali inayopelekea abiria wengi wanaotumia usafiri huo kuona kama ni kawaida kwa wao kutopatiwa tiketi.

Akizungumza ofisini kwake, Ofisa Mfawidhi wa SUMATARA kanda, Amani Shamaje, alisema kuwa wamedhamiria kukomesha tabia hiyo ambayo imekuwa kero kwa abiria wengi.

Shamaje alisema kuwa tatizo hilo lilikuwepo pia kwa mabasi yafanyayo safari kwenda wilayani, lakini hivi sasa limekwisha baada ya SUMATRA kuingilia kati na kuanza kuyakamata mabasi hayo na kutoza faini ya shilingi 250,000 kwa kila basi lililokuwa halitoi tiketi kwa abiria.

"Hivi sasa mabasi mengi yafanyayo safari za kwenda wilayani yamekuwa yanatoa tiketi kwa abiria...tatizo tulilonalo sasa ni utoaji wa tiketi kwa daladala zifanyazo safari hapa jijini Mbeya" alisema Shamaje.

Aliongeza kuwa waliamua kwanza kutilia mkazo suala la uvaaji wa sare kwa madereva na makondakta wa daladala na pia kupiga marufuku usimamaji kwa sehemu zisizo kuwa na vituo ambapo wameweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Ofisa Mfawidhi huyo wa SUMATRA kanda ya nyanda za juu kusini, alisema utoaji wa tiketi kwa abiria wa daladala jijini Mbeya, limekuwa ni tatizo linalowasumbua kwa muda mrefu na wameamua kujipanga ili kuhakikisha kuwa wanalimaliza.

Alisema kuanzia sasa daladala yoyote inayofanya safari zake jijini Mbeya, ambayo itakuwa haitoi tiketi kwa abiria itakuwa inatozwa faini ya shilingi 250,000 au kifungo cha kuanzia mwaka mmoja ama kisichopungua miwili au adhabu zote kwa mpigo.

Katika hatua nyingine, Shamaje alisema kuwa wanaandaa mkakati wa kuwadhibiti madereva wa daladala zinazotoka jijini Mbeya kwenda mji mdogo wa Mbalizi, ambazo zimekuwa hazifiki mwisho wa safari na badala yake kuishia eneo la Iyunga na hivyo kupelekea usumbufu kwa abiria.

Alisema kuwa watakutana na Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani mkoa wa Mbeya, Ezekiel Mgeni, ili kuangalia njia sahihi za kukomesha tabia hiyo ambayo hufanywa kuanzia saa 12:00 jioni ambayo imekuwa inapelekea abiria walazimike kupanda mabasi mawili tofauti ili kukamilisha safari

."Huu ni usumbufu kwa abiria kwani unakuta gari limeandikwa kuwa linakwenda Mbalizi, lakini likifika Iyunga abiria wanaambiwa kuwa hapo ndio mwisho wa safari...hii ni usumbufu kwani huwalazimu abiria kupanda daladala lingine ili kuwawezesha kukamilisha safari" alisema Shemaje.