Wednesday, June 3, 2009

CHUNYA WAKAMATA MAKOKORO YENYE THAMANI YA ZAIDI YA SH.MILIONI 20

MAKOKORO 103 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 20,600,000, yamekamatwa katika maeneo ya Isanzu na Udinde yaliyopo pembezoni mwa Ziwa Rukwa, wilayani Chunya.

Imeelezwa kuwa wamiliki wa makokoro hayo hawakuweza kutiwa mbaroni baada ya kuwahi kukimbia na kuyatelekeza makokoro hayo.

Akizungumza Ofisa Uvuvi wa wilaya hiyo, Christina Potta, alisema kuwa operesheni ya kuyakamata makokoro hayo ilifanyika kati ya Mei 3, na hadi 14, mwaka huu katika maeneo hayo yaliyopo Ziwa Rukwa, upande wa wilaya ya Chunya.

Christina alisema kuwa matumizi ya makokoro huwa yanapelekea upungufu wa samaki kwani nyavu za aina hiyo (makokoro), kutokana na kuwa na macho madogo zinapovutwa huharibu viota, mayai, vifaranga vya samaki na hivyo kuua vizazi vya samaki.

Aliongeza kuwa katika zoezi hilo, wilaya hiyo ilishirikiana na kikosi cha doria cha uvuvi cha Kanda ya Kasanga, kilichopo mkoani Rukwa.

"Kazi ya kutupa makokoro ziwa Rukwa huwa inafanywa nyakati za usiku, hivyo hutuwia vigumu kuwatia mbaroni watuhumiwa na huwa tukienda mchana huwa ntunafanikiwa kuyakukuta makokoro lakini wamiliki wake huwa wanafanikiwa kukimbia" alisema Christina.

Ofisa Uvuvi huyo wa wilaya alisema ili kukabiriana na wavuvi ambao wamekuwa watumiaji wakubwa wa makokoro, wilaya imekuwa inajitahidi kutoa elimu kwa wananchi juu athari za makokoro.Christina alisema:

"Tunaendelea kushirikiana na viongozi wa vijiji katika utoaji elimu hali iliyopelekea baadhi ya wavuvi kwa hiyari yao wenyewe, kuamua kuanza kusalimisha makokoro waliyokuwa wanayatumia".

Aliongeza kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kuwa watumiaji wa makokoro hayo kwa kutumia simu za kiganjani, wamekuwa wanapeana taarifa kila unapofanyika msako hali inayowawia vigumu kuwatia mbaroni watuhumiwa ili kuwafikisha mbele ya sheria.

Alisema wilaya katika kukabiriana na tatizo hilo, imefanikiwa kukamilisha matengenzo ya Boti ya doria ambayo tayari imetumbukizwa kwenye Ziwa Rukwa, ambayo itasaidia sana kukabiriana na wavuvi wanaotumia makokoro katika shughuli zao za uvuvi.

No comments:

Post a Comment