WAZIRI wa Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Selina Kombani, amesema kuwa ofisi yake imepokea taarifa za kuwepo malumbano kati ya watendaji na viongozi wa siasa jijini Mbeya.
Alisema lakini serikali haiwezi kuzifanyia kazi hizo za malalamiko bila ya kuzifanyia utafiti, hivyo kuwataka waliopeleka taarifa hizo kuvuta subira.
“Nawaomba wale walioniletea taarifa hizi ofisini kwangu kuwa na subira ili niweze kuniwezesha kufanya utafiti kwa nia ya kutoa majibu yaliyo sahihi” alisema Selina.
Hayo aliyasema jana mjini hapa, mara baada ya kufungua semina ya madiwani wanawake mkoani hapa,katika ukumbi wa Benjamini Mkapa yenye nia ya kuwawezesha kuwa na ujasiri katika kugombea nafasi za uongozi.
Waziri wa TAMISEMI alisema ofisi yake ilishapokea taarifa za kuwepo malumbano kati ya watendaji na viongozi wa kisiasa wa halmashauri ya jiji la Mbeya.
Aliongeza kuwa hatua za awali zilizochukuliwa ni kufanya utafiti wa chanzo cha malumbano hayo, ambapo baada ya kubainika chanzo cha tatizo hilo ndipo utatolewa uamuzi utakaokuwa na nia ya kuutendea haki kila upande.Selina alisema:
”Lengo la TAMISEMI kukaa kimya muda mrefu bila ya kutoa maamuzi ya malalamiko hayo (hakutaja kundi lililopeleka kwakwe), ni kuhakikisha uamuzi unaotolewa hauumizi upande mmoja au kuwagawa wahusika”.
Waziri huyo alikiri kuwa ni kweli ofisi ama sehemu yoyote inayokuwa na malumbano, shughuli za utendaji hushuka lakini hilo haliwezi kuifanya serikali ikatoa maamuzi yasiyofanyiwa utafiti wa kina hivyo kuwataka wananchi kuwa wavumilivu.
“Nakubaliana nanyi kuwa sehemu kunapokuwa na malumbano ya namna hii kazi nyingi zinafanyika kwa kiwango cha chini…lakini kwa kuwa hazijasimama kabisa,niwaombe wananchi wa Mbeya na taifa kwa ujumla kuvuta subira ili uamuzi utakaotolewa uwe na manufaa kwa wote” alisema Selina.
Alisema utaratibu uliopo TAMISEMI ni kuwa wanafanyia kazi maelezo yaliyotolewa na pande zote mbili kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na maofisa wake na kwamba vikao vitaketi na kupitia taarifa hiyo ili kufikia uamuzi.
Malumbano yaliyofikishwa TAMISEMI ni kati ya mkurugenzi wa jiji la Mbeya, Elibeth Munuo na Meya wake Athanas Kapunga, ambapo kwa nyakati tofauti kila mmoja amekuwa akimlaumu mwenzake kuwa ni chanzo cha matatizo mbalimbali katika halmashauri hiyo.
Wednesday, June 3, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment