HALMASHAURI ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, ni miongoni mwa halmashauri 54 nchini, zilizofanikiwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka wa fedha 2007/2008.
Hilo limetokana na halmashauri kuwa na watumishi wenye uwezo na pia kitengo cha ukaguzi wa ndani kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika idara za halmashauri hiyo.
Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo, Saimon Minja, aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumzia kuhusu jitihada zinazofanywa na kitengo hicho muhimu katika kuhakikisha halmashauri hiyo inasonga mbele.
Minja alisema kwa kitengo hicho kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, huwa inasaidia wahusika kurekebisha makosa yao na hivyo anapokuja mkaguzi wa nje, huwa anakuta matatizo yote yameisharekebishwa.
"Pia kitu kingine kilichotusaidia kupata hati safi ni ushirikiano mkubwa uliopo kati ya kitengo cha ukaguzi wa ukaguzi wa ndani na Mkurugenzi Maurice Sapanjo, hali ambayo inafanya mazingira ya kazi kuwa rahisi" alisema Minja.
Aliongeza kuwa Mkurugenzi Sapanjo amekuwa anatumia taarifa za kitengo hicho kuwakemea na pia kuwashauri wakuu wa idara kutokana na taarifa anazokuwa amefikishwa mezani pake.
Alisema Changamoto waliyonayo hivi sasa ni ukubwa wa wilaya hiyo hivyo kuwa kikwazo kwao kuweza kufika maeneo yote ya wilaya hiyo kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa ndani wa hesabu.
Ofisa huyo wa wilaya alisema vile vile kitengo hicho cha ukaguzi wa ndani hakina usafiri hali inayowalazimu kuomba magari kutoka idara nyigine, na inapotokea magari hayo kuwa na kazi hulazimika kusubiri ili kwenda kutekeleza majukumu yao.
Minja alisema:"Kuna dhana potofu iliyopo wilayani hapa kwa baadhi ya watu wakiwemo wana-siasa kuwa Mkaguzi wa ndani anatakiwa kuwakamata watu wanaobainika kufuja fedha za halmashauri, kitu ambacho siyo sahihi".
Alifafanua zaidi kauli yake hiyo kuwa wao wanachokifanya mara baada ya kubaini ubadhirifu wa fedha ndani ya idara yoyote huwa wanazifikishga taarifa kwa Mkurugenzi kwa hatua zaidi na wao huwa hawana uwezo wa kuwa polisi wa kuwakamata wabadhirifu hao.
Minja aliongeza kuwa pia kitengo hicho kinakabiriwa na upungufu wa watumishi kwani kinao wawili tu na mmoja hivi sasa yupo masomoni, hali inayofanya utendaji wa kazi kuwa mgumu hasa ukizingatia kuwa wilaya ina eneo kubwa kuliko wilaya nyigine zote mkoani hapa.
Wednesday, June 3, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment