TAASISI ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST), imeanza kutekeleza agizo la Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Peter Msolla, la kuhakikisha kuwa wanaongeza udahili wa wanafunzi wa kike kujiunga chuoni hapo.
Hadi sasa walimu wa taasisi hiyo wamezitembelea shule za sekondari 21 mkoani hapa, ili kutoa elimu kwa wanafunzi wa kike kupenda kusoma masomo ya sayansi,Hisabati na ufundi.
Profesa Msolla alitoa agizo hilo hivi karibuni wakati akizindua shahada katika fani za biashara na uhandisi katika fani za ujenzi, umeme, Mitambo na Usanifu wa Majengo, katika taasisi hiyo.
Mkuu wa MIST Profesa Joseph Msambichaka, aliyasema hayo jana, wakati akielezea kuhusu hatua ya taasisi hiyo kuandaa semina ya siku tatu kwa kushirikiana na asasi ya Peace Corps Tanzania ya nchini Marekani, kwa ajili ya kumuwezesha mtoto wa kike kuyapenda masomo hayo.
Semina hiyo inashirikisha wanafunzi wa kike 80, wa shule za msingi na sekondari kutoka wilaya wilaya zote za mkoa wa Mbeya, na wanafundishwa na wataalam saba wa kujitolea, kutoka Peace Corps Tanzania.
Profesa Msambichaka alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni kuwa wanafunzi wa kike wamekuwa na tabia ya kuyakimbia masomo ya sayansi na kuwaachia watoto wa kikume madai kuwa masomo hayo ni magumu kitu ambacho siyo kweli.
Alisema kuwa hivi sasa MIST inao utaratibu wa kutoa mafunzo maalumu kwa ajili ya somo la Hisabati kwa watoto wa kike wanaokuwa wamemaliza elimu ya sekondari.
"Wale wanaokuwa wamefaulu vizuri huwa serikali inaingia gharama ya kuwasomesha kwa muda wote wanaokuwepo hapa taasisi lengo likiwa ni kuwahamasisha kuyapenda masomo ya sayansi" alisema Msambichaka.
Profesa Msambichaka alisema kuwa mwaka 2008, wanafunzi wa kike 13 walifanya masomo hayo maalumu, ambapo kwa mwaka jana waliojitokeza walikuwa ni zaidi ya 50.
Nao washiriki wa semina hiyo, wakizungumza kwa nyakati tofauti na Uhuru, walisema kuwa wanashukuru kwa kupata semina hiyo kwani ni ukweli kuwa watoto wa kike wapo nyuma.
Walisema kuwa wazazi wengi huwa wanawaona watoto wa kiume kuwa ndio wanaopaswa kusoma na wao kupenda kufanyishwa kazi za nyumbani hivyo huwa na muda kidogo wa kujisomea tofauti na wenzao wanaume.
"Tunataka kuiambia jamii kuwa tulikuwa nyuma kutokana na mfumo dume uliojenga kwa muda mrefu...watoto wa kike tulikuwa tunaonekana kwamba hatuwezi kusoma kwani mzazi aliyekuwa anamsomsemesha mtoto wa kike alikuwa akionekana anapoteza muda" walisema.
Tuesday, June 16, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment