Friday, July 10, 2009

DAWA ZA KUONGEZA MATITI,HIPS NA MAKALIO ZAKAMATWA IRINGA

MKAGUZI wa Dawa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kanda ya nyanda za juu kusini, Paul Sonda, amesema kuwa wamefanya ukaguzi wa ghafla na kulibaini duka moja mkoani Iringa, linalouza dawa za kuongeza matiti, makalio na Hips kwa wanawake.

Imeelezwa kuwa TFDA iliamua kufanya ukaguzi huo wa kawaida baada ya kupewa taarifa na raia wema kuwa duka hilo linauza dawa hizo ambazo zimetengezwa nchini China.

Akizungumza jana Sonda alisema kuwa baada ya kufanya ukaguzi huo walibaini kwamba dawa zote zinazouzwa dukani humo pamoja na jengo lenyewe vyote havijasajiliwa na TFDA.

“Tuliwahoji wauzaji ili kutaka kujua sehemu walikozinunua dawa hizo ambazo zimeandikwa kwa lugha ya Kichina lakini hawakuweza kuweleza kwani hata nyaraka walizonunulia hawakuwa nazo” alisema Sonda.

Alisema TFDA huwa wanasajili dawa zenye maandishi ya Kiingereza, Kiswahili ama zilizoandikwa kwa lugha zote hizo mbili lakini siyo nje ya hapo.

Mkaguzi huyo wa dawa kanda hii aliongeza kuwa dawa inaweza iikawa imeandikwa kwa lugha yoyote ile duniani lakini sharti ni kuwa lazima kuwepo na tafsiri ya maandishi hayo kwa Kiingereza ama Kiswahili.

Sonda alisema kuwa walitoa elimu kwa wauzaji wa duka hilo kuhusu umuhimu wa kusajili jengo hilo pamoja na bidhaa wanazouza ambapo walitoa ushirikiano mzuri.

Alisema:”Baadaye tulizichukua dawa hizo za kuongeza matiti, makalio na Hips na kuondoka nazo kwa kujibu wa taratibu zilizopo na tulikwenda kumkabidhi Mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuziteketeza”.

Aliongeza kuwa hawakuweza kujua thamani halisi ya dawa hizo lakini zilikuwa nyingi na kuwa kwa ukaguzi walioufanya katika mikoa mingine ya Mbeya, Rukwa na Ruvuma hawajaweza kuzibaini dawa za aina hiyo.

No comments:

Post a Comment