MWANAFUNZI wa kidato cha nne,shule ya sekondari Iyunga,jijini Mbeya amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari eneo la Nzovwe, akiwa anatembea pembezoni mwa barabara.
Ajali hiyo iliyohusisha gari ambayo ni daladala yenye namba za usajili T.129 AMD aina ya Toyota Hiace,ikiendeshwa na dereva Japhet Mwile, ilitokea jana saa 2:00 asubuhi katika barabara ya Mbeya kwenda Tunduma.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya,Advocate Nyombi, akizungumza jana ofisini kwake, alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Hery Mlengule.
Nyombi alisema kuwa daladala hiyo ikiwa na abiria ndani yake ilikuwa inaelekea mji mdogo wa Mbalizi na mara baada ya ajalib hiyo, dereva pamoja na gari walipelekwa kituo kikuu cha polisi.
Uchunguzi zaidi juu ya ajali hiyo unaendelea kufanywa ili kujua chanzo cha ajali hiyo.
Katika tukio lingine lililotokea eneo la Forest Mpya, jijini hapa,mtoto mchanga wa kike mwenye umri kati ya wiki moja ama mbili aliokotwa akiwa ametupwa katika mfereji wa maji machafu na mtu asiyefahamika.
Kwa mujibu wa Kamanda Nyombi, tukio hilo lilitokea jana saa 11:00 jioni katika mtaa wa Kilimani uliopo eneo hilo.
Alisema kuwa mtoto huyo aliokotwa akiwa hai na Esther Mwakalebele, ambaye alikuwa anamwagilia bustani yake ya mboga mboga iliyopo jirani na mtaro huo wa maji machafu.
Nyombi alisema kichanga huyo yupo hai na anahifadhiwa hospitali ya Rufani Mbeya, kitengo cha Wazazi Meta na msako wa kumsaka mwanamke aliyefanya kitendo hicho cha kikatili unaendelea kufanywa.
Tuesday, July 7, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment