Sunday, July 19, 2009

POLISI WATATU WATUPWA LUPANGO KYELA

POLISI watatu wilayani Kyela, wanashikiliwa kwa tuhuma za kuwa chanzo cha vurugu zilizotekea wilayani humo mara baada ya raia Lucas Mwaipopo,mkazi wa Mbugani kuuawa kwa kinachodaiwa ni kipigo kutoka kwa polisi.

Vurugu hizo zilipelekea wananchi zaidi ya 500 kuvamia na kupiga mawe kituo cha polisi, kuchoma moto mahakama ya Mwanzo ya Kyela mjini na pia kufanya uharibu wa mali katika ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo.

Polisi hao watatu wanaoshikiliwa ambao wote wana cheo cha Masajenti kutoka kitengo cha upelelezi wametajwa kuwa ni John mwenye namba D.4067, Joseph mwenye namba F.4849 na Mussa mwenye namba F.5753.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi alisema jana kuwa polisi hao watatu wanashikiliwa ili kuhojiwa kuweza kupata chanzo cha vurugu hizo zilizotokea wilayani humo na kupelekea polisi kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwadhibiti wananchi hao.

Alisema kuwa endapo polisi hao watatu wanaotuhumiwa kuwa chanzo cha kuzuka kwa vurugu hizo, wakibainika kuwa ni kweli watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kuwa fundisho kwa wengine.

Nyombi alisema kuwa watu 96 walikamatwa kwa tuhuma za kuchochea vurugu hizo, ambapo walihojiwa na kumi na watano (15), kati yo wamefikishwa mahakamani jana kwa kosa la kufanya vurugu na kuvamia kituo cha polisi.

Aliwataja polisi wanane waliojeruhiwa kwa kupigwa mawe kuwa ni mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Kyela Richard Mchomvu, E.9945 PC Julius, G. 54 PC Nyanda, E.7201 PC Timoth, E.1787 Koplo Robert, D.9713 Koplo Sarafini, E.3732 Koplo Travael, na E.8631 Sajent Mwita.

Aidha, magari mawili ya polisi yenye nmba za usajili PT.0798, PT. 0799 yote aina ya Lanlover yaliharibiwa kwa kupigwa mawe huku magari mengine ni T.646 AYL aina ya Landlover mali ya Daniel Mwambulukutu na T. 279 ARJ aina ya Toyota Hiace.

Kamanda Nyombi alisema kuwa katika watu waliojeruhiwa katika vurugu hizo yumo Ofisa Maeneleo ya Jamii wilaya ya Kyela, Nulusigwa Mwakigonja ambaye gari lake lenye namba za usajili T.573 AFA lilipoteza uelekeo na kugonga mti ambapo limeharibika vibaya.

Taarifa nyigine zilizopatikana kutoka hopitali ya Rufani Mbeya, zilidai kuwa majeruhi Jackob Antony (24), ambaye alipigwa risasi iliyoingia tumboni na kutokea kwenye kalio lake la upande wa kulia alikuwa anplekwa chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuondolewa risasi.

Kufuatia vurugu hizo polisi juzi walilazimika kutangaza hali ya hatari na kuwataka wananchi kuwepo majumbani mwao ifikapo saa 1:30 usiku hali iliyopelekea mji huo wa mpakani na nchi jirani ya Malawi kupooza huku mitaa yote ikiwa haina watu.

Ni Mtizamo Tu ilishuhudia baadhi ya wateja waliokutwa katika baa ya Half London, iliyopo mjini humo wakipewa misukosuko kwa kukaidi kutii amri hiyo baada ya kukutwa wakiendelea kunywa vinywaji.

Hali hiyo ilipelekea wageni wengi waliochelewa kupta chakula cha jioni kulazimika kulala njaa kwani hakuna hotel ama baa yoyote iliyokuwa inafanya kazi kutokana na amri hiyo ya hatari.

Kituko kingine kilikuwa ni pale msichana aliyetajwa kwa jina la Jenny Chawe, ambaye alikuwa salon iitwayo Mariam iliyopo Kyela mjini akirembwa kujiandaa na sherehe ya kuagwa, naye kupotea kufuatia vurugu hizo hali iliyopelekea ndugu zake kuanza kuhaha kumtafuta mitaani.

Pia baadhi ya wanawake walikutwa barabarani wakiwa wanahaha kuwatafuta watoto wao baada ya kupotezana nao kufuatia vurugu hizo, lakini walifanikiwa kuwapata baadaye hali ilipotulia.

No comments:

Post a Comment