Friday, July 10, 2009

MKUU WA ST.AGGREY SEKONDARI ABAKA MWANAFUNZI

MKUU wa shule ya sekondari ya St.Aggrey, jijini Mbeya Henry David Chelula, amefikishwa mahakama ya mkoa wa Mbeya, akikabiriwa na kosa la kutaka kumbaka mwanafunzi wa kike wa kidato cha nne shuleni hapo.

Chelula alikamatwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani hapa baada ya kuwekewa mtego.

Kesi hiyo ya jinai namba 135 ya mwaka huu ipo chini ya mwendesha mashtaka, Wakili wa serikali Keneth Sekwao na inasikilizwa na Hakimu mkazi Deborah Ndyekura.

Ilidai mahakamani hapo kuwa Julai 2,mwaka huu saa 11:00 jioni katika baa iliyo pia na nyumba ya kulala wageni iitwayo New M. Jokes iliyopo eneo la Maendeleo jijini Mbeya, chumba namba 11, mtuhumiwa Chelula alimdai rushwa ya ngono mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa), mwenye umri wa miaka 18.

Ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo alimdai mwanafunzi huyo wa kike anayesoma shule ya sekondari ya St.Aggrey ambayo yeye ni Mkuu wa shule, rushwa ya ngono kama sharti la kutoa huduma muhimu.

Chelula alikana shtaka hilo na yupo nje kwa dhamana hadi Julai 17,mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Wakati huo huo Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mbeya, Respick Ndowo, alisema kuwa taasisi hiyo inaendelea na uchunguzi kuhusiana na rushwa ya ngono kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Ndowo alisema mtuhumiwa Chelula amefikishwa mahakamani ya mkoa Mbeya na ofisi ya mwanasheria wa serikali akikabiriwa na kosa la hilo la kubaka ambalo ni kesi ya jinai iliyopewa namba 135 ya mwaka huu.

No comments:

Post a Comment