Friday, July 10, 2009

JWTZ WAFANYA USAFI KATIKA MASOKO JIJINI MBEYA

WAFANYABIASHARA wa masoko ya Matola na Uhindini, yaliyopo jijini Mbeya, wamelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kufanya usafi mkubwa katika masoko hayo jana.

Walisema kuwa hatua hiyo imezidi kuonyesha jinsi JWTZ linavyothamini na kuisaidia jamii katika mambo mengine ya kijamii mbali ya ulinzi wa mipaka ya nchi yetu.

Akizungumza na Uhuru kwa niaba ya wenzake, Makamu Mwenyekiti wa soko la Matola, Abdallah Shaibu, alisema wanalishukuru jeshi kwa uamuzi wa kwenda kuwafanyia usafi katika soko lao.

“Hii ni changamoto kubwa sana kwetu wafanyabiashara sokoni hapa tuliyopewa na JWTZ ya kuzingatia usafi wa soko hili kwa afya zetu na wananchi wanaokuja kununua mahitaji mbalimbali sokoni hapa” alisema Shaibu.

Aliongeza kuwa hali hiyo itasababisha wafanyabiashara hao waone kuwa usafi wa maeneo yanayolizunguka soko hilo ni muhimu na siyo kusubiria hadi wageni kutoka nje (JWTZ), ndio waende kuwafanyia kazi hiyo.

Shaibu aliwashauri wafanyabiashara wa masoko hayo ya Uhindini na Matola kuiga mfano huo wa kuzingatia usafi na kuyatunza maeneo yao kama walivyoonyeshwa na JWTZ na siyo kubweteka na kujua kazi ya usafi katika masoko hayo haiwahusu wao bali wafanyakazi wa halmashauri ya jiji la Mbeya.

Shaibu alisema:”Tunalishukuru sana JWTZ kwa uamuzi huu wa busara waliouchukua wa kuzijali afya zetu…walifika hapa saa 1:30 asubuhi na baada ya kufanya usafi soko lote waliondoka saa 3:30 asubuhi”.

No comments:

Post a Comment