MUZIKI wa Reggae umetokea kujipatia mashabiki na wapenzi wengi duniani kutokana na mashairi yake siku zote kugusa maisha halisi ya binadamu.
Kifupi unalenga ukweli halisiNa ndio maana leo hii unapomtaja mwanamuziki mahiri na mfalme wa Reggae, marehemu Robert Nesta Marley maarufu zaidi kwa jina la Bob Marley, hata mtoto mdogo wa miaka mitano hawezi kupata kigugumizi kukueleza kuwa anazipenda nyimbo zake.
Lakini pia kuna waimbaji wengine mahiri wa muziki huu ambao mara nyingi wanamuziki wake hupenda kuziachia nywele zao kichwani kuwa ndefu yaani kufuga Rasta, kama kitambulisho cha muziki huo.Hata hivyo kuna wanamuziki wengine wa muziki huu hawana Rasta.
Mmoja wa waimbaji hao ambao nao wamejipatia sifa na kuutangaza muziki huu wa Reggae na kupelekea kujipatia umaarufu duniani ni marehemu Joseph Hill, kiongozi wa kundi la Culture.
Hill alikuwa ni kiongozi wa kundi hilo la Culture lililokuwa linaundwa na wasanii wakongwe ambalo lilitokea kujipatia sifa kubwa nchini Jamaika na duniani kwa jumla.
Mnamo Agosti 19, mwaka 2006, wapenzi na mashabiki wa reggae walipatwa na mshituko mkubwa kufuatia kifo cha msanii huyu mahiri aliyekuwa na sauti ya kipekee iliyoweza kumtoa nyoka pangani.
Hill alikutwa na mauti mjini Berlin nchi Ujerumani, baada ya kuugua ghafla akiwa katikati ya ziara ya kimuziki barani Ulaya na kundi na kundi lake la Culture.
Kutokana na mchango wake mkubwa Hill alitunukiwa tuzo nyingi ikiwemo ile iliyojulikana kama ‘Jamaika Reggae Walk of Fame and a 2005 Independence Award’ aliyotunukiwa na Waziri Mkuu wa Jamaika.
Kifupi ni kuwa unapokuwa unawaongelea magwiji wa muziki wa Reggae waliowahi kutokea hapa duniani, basi ni wazi lazima utalitaja pia jina la Hill kuwa miongoni mwao na hilo halina ubishi.
Kundi la Culture lililoundwa mnamo mwaka 1976, na kujizolea umaarufu mkubwa huku likijulikana pia kama Mitume ya Afrika, lilikuwa linaundwa na wasanii wakali wakiwemo Joseph Hill, Albert Walker na Kenneth Dayes.
Hill alikuwa ni msanii pekee ndani ya kundi hilo aliyekuwa na uzoefu wa mambo ya Studio, baada ya kuwa amewahi kufanya kazi katika studio ya Coxone Dodd's akiwa mmoja wa waandaaji wa nyimbo za kundi lililoitwa Soul Defenders mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Muda mfupi baada ya kuanzishwa kwa kundi la Culture, lilianza kufanya kazi na mtayarishaji wa muziki aitwaye Joe Gibbs akiwa na Injinia wake Errol Thompson. Wakiwa na Gibbs walifanikiwa kurekodi albamu mbili zilizojipatia umaarufu mkubwa.
Mara baada ya kutolewa kwa albamu hizi mbili ambazo zilikuwa na mtazamo mchanganyiko wa historia ya Jamaika, na mtazamo mpya wa mabadiliko ya hali ya hewa. Baada ya kupata mafaniko wakiwa na Gibbs, kundi hilo lilihama na kwenda kufanya kazi na mtayarishaji mwingine aliyejulikana kwa jina la Sonia Pottinger.
Culture pia walianza kufanya kazi na wanamuziki wengine mahiri waliopo kama Robbie Shakespeare, Sly Dunbar, Ansel Collins na Cedric Brooks.Kampuni ya kurekodi ya Virgin ilichukua albamu yao iliyowafanya (Culture) , wazidi kuwa maarufu na kupata mashabiki hadi nje ya Jamaika.
Mwaka 1982 waimbaji watatu wa kundi hilo waliojiondoa na kuanza maisha yao kivyao, ambapo Joseph Hill aliendelea kutumia jina la Culture lakini baadaye mwaka 1986 waliungana tena na kurekodi albamu mbili zilizojizolea umaarufu mkubwa za 'Culture in Culture' na 'Culture at Work'.
Baadaye mwaka 1993 Kenneth Dayes aliondoka katika kundi na kubadiliwa kwa muda na muimbaji kutoka kundi la Dub Mystic, ambaye.
Wakiwa na Dub Mystic, Culture walifikia mafaniko ya juu kimuziki baada ya kuachia albamu za 'One Stone' na ‘Trust Me' na live albamu iliyokwenda kwa jina la 'Cultural Livity'. Baada ya kundi hilo kudumu kwa muda wa miaka 27,Joseph Hill na wenzake hawakuonyesha dalili za kushuka kiwango chao kimuziki.
Kundi la Culture liliendelea kuwa imara likiwa na msimamo wa kudumisha ukweli kuhusu asili ya muziki wa Reggae lakini pia muda mwingine likiingiza milio na sauti mpya katika muziki wao.
Wanamuziki wa kundi la Culture wameonyesha njia kuwa ni moja ya kundi bora la muziki wa Reggae lililoweza kutawala kuanzia katika utunzi wa mashairi ya albamu albamu zao hadi katika kulitawala jukwaa.
Sunday, July 19, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment