Tuesday, July 7, 2009

SAMAKI WAPUNGUA ZIWA RUKWA-MBOZI

UVUVI haramu unaondelea kufanyika katika Ziwa Rukwa,upande wa wilaya Mbozi, umepelekea kupunguza kiwango cha uvuvi ziwani humo,imeelezwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Mbozi,Levisson Chilewa, alisema hilo limebainika baada ya kuona samaki wengi wanaovuliwa kutoka ziwani humo ni wale wadogo (wachanga).

Chilewa alisema kufuatia hali hiyo walitoa ombi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili wafunge shughuli za uvuvi kwa miezi minne yaani kuanzia mwezi Januari hadi Aprili mwaka huu ili samaki waweze kuzaliana.

“Tuliona kuwa kipindi hiki ndio ambacho samaki huwa wanazaliana na kukua, hivyo tungeweza kutatua tatizo hili la upungufu wa samaki katika Ziwa hili upande wa Mbozi” alisema Chilewa.

Aliongeza kuwa njia nyingine wanayoitumia katika kukabiriana na hatari ya samaki kutoweka kabisa Ziwani humo, ni kujenga mabwawa 104 ya kufugia samaki ambapo katika viwanja vya ofisi ya halmashauri hiyo wanalo bwawa moja.

Mkurugenzi alisema kuwa bwawa hilo la halmashauri huwa linatumika kwa ajili kuzalisha samaki aina ya Perege ambao huwauza kwa wananchi, taasisi za kiserikali na zile zisizokuwa za kiserikali.

“Nia yetu ni kuhakikisha kuwa wananchi wananchi wanaendelea kutumia Samaki ili kuongeza lishe pia kujioongezea kipato zaidi” alisema Chilewa.

Aliongeza kuwa halmashauri imetengeneza boti ya kufanyia doria yenye thamani shilingi milioni 4.8 huku injini yake ikiwa na thamani ya shilingi milioni 2.8 kwa ajili ya kukabiriana na wavuvi haramu katika Ziwa hilo.

Chilewa alisema kwa kutumia boti hilo wameweza kukamata makokoro 37 na nyavu 110 zenye macho madogo ambazo hutumiwa na wavuvi haramu ambao wamepelekea kupungua kwa samaki Ziwani humo.

Ziwa Rukwa limepitia katika wilaya za Chunya na Mbozi kwa upande wa mkoa wa Mbeya na wilaya za Mpanda pamoja na Sumbawanga Vijijini,kwa mkoa wa Rukwa.

No comments:

Post a Comment