Sunday, July 19, 2009

RAS MKOA WA MBEYA AWATIMUA WAANDISHI WA HABARI

WAANDISHI wa habari kutoka vyombo mbalimbali, jana walishindwa kuhudhuria kikao cha Mkuu wa mkoa wa Mbeya,John Mwakipesile na Jaji Mkuu Agustino Ramadhan, baada ya Katibu Tawala wa mkoa (RAS), Beatha Swai kuwazuia mlangoni.

Tukio hilo lilitokea jana saa 3:00 asubuhi, mara baada ya waandishi wa habari kufika hapo kuitikia wito uliotolewa na Ofisa Uhusiano wa Mahakama Kuu (PRO), Nurdin Ndimbe kuhudhuria kikao hicho bila kukosa.

Waandishi hao zaidi ya saba, walifika ofisi hizo muda waliotakiwa na walipotaka kuingia katika kikao hicho, walikutana nja kikwazo hicho kutoka kwa RAS Beatha akishirikiana na Msaidizi wa Mkuu wa mkoa (DPS), ambaye jina lake halikuweza kujulikana.

Hatua hiyo ni tofauti na taarifa iliyotolewa na Afisa Uhusiano huyo wa Mahakama Kuu, Ndimbe ambaye aliwaeleza waandishi kuwa wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika ziara ya Jaji kuanzia ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kwingineko.

Vikwazo hivyo vilianzia kwa Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa (DPS) ambaye aliwaeleza waandishi kuwa hakuwa na taarifa ya waandishi kutakiwa kuingia katika ofisi hizo na kuwataka watoke nje wakasubiri.

Hata hivyo juhudi za waandishi kujaribu kumuelekeza umuhimu wa wao kuhudhuria mazungumzo baina ya Mkuu wa Mkoa na Jaji Mkuu ziligonga mwamba baada ya Katibu Tawala, Beatha kusimama mlangoni na kuwazuia baadhi ya waandishi kwa kuwasukumia nje ya ofisi.

Baada ya kuwepo kwa kutoelewana baina ya waandishi, msaidizi wa mkuu wa mkoa na Katibu Tawala, Afisa habari wa mahakama, Ndimbe aliwaomba waandishi wasubiri nje huku naye akiwa haelewi kinachoendelea na sababu za waandishi kuzuiwa.

Baadhi ya waandishi walilalamikia kitendo cha Swai kwa madai kuwa yeye pamoja Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa wamekuwa na tabia ya kuwazuia waandishi na wakati mwingine kudai hawaruhusu kumuona Mkuu wa Mkoa bila ya kuwa na miadi naye.

Lakini tukio hilo liliwasikitisha waandishi wengi kwani ni tofauti na ushirikiano mkubwa alionao Mwakipesile tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo, kwani amekuwa akiwataka waandishi kumuona muda wowote wanapokuwa na jambo la dhalura.

“Hawa wanatushangaza, sisi kumuona Mkuu wa Mkoa lazima tuwe na miadi hata kama kuna jambo la dharura, lakini ofisi ya Mkuu wa Mkoa huwa inaita waandishi bila ya kuweka miadi, hii ni ajabu kabisa” alisema.

Jaji Ramadhani jana alikuwa Mkoani Mbeya kwa ziara ya siku moja ambapo aliwasili Mkoani Mbeya akitokea Mkoani Rukwa.

No comments:

Post a Comment