Thursday, July 23, 2009

MARY MWANJELWA AJITOLEA KUSOMESHA WATOTO YATIMA WANANE MBEYA

MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake (UWT), kutoka mkoa wa Mbeya, Mary Mwanjelwa, amejitolea kusomesha watoto yatima wa kike wanane waliofaulu mtihani wa darasa la saba, kutoka wilaya zote mkoani hapa, lakini hawana uwezo wa kusomeshwa sekondari.

Hivyo amezitaka kamati za Utekelezaji za UWT za wilaya hizo, kufanya mchakato bila ya upendeleo ili kuwapata watoto hao yatima ambao yeye atawajibika kuwalipia ada na mahitaji yote muhimu katika sekondari za kata.

"Jukumu la kuwalea watoto hawa yatima ni letu sisi wanawake wote...serikali na taifa kwa jumla wameonyesha kuwajali watoto hawa hivyo imefika kipindi na sisi tuone jukumu hili ni letu" alisema Mary.

Hayo aliyasema katika ziara yake ya kushukuru kwa kuchaguliwa katika nafasi hiyo na pia kuangalia uhai wa jumuia ya UWT na Chama Cha Mapinduzi kwa jumla.

Ameongozana na Katibu wa UWT mkoa wa Mbeya, Mwanaidy Mbisha na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UWT mkoani hapa, Florence Mwakanyamale.

Mary alisema mwanamke ndiye uhai wa jamii yoyote ile na ndio maana hata kwenye suala la uzazi wa Mpango iwapo mwanamke atakataa kushiriki ni wazi suala hilo halitawezekana.

Aliwataka wanawake mkoani Mbeya kuwajali na kuwathamini watioto yatima waliopo katika maeneo yao ili nao waweze kujiona siyo wanyonge kwa vile tu walipoteza wazazi wao wote wawili.Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la UWT Taifa alisema:

"Hivyo nawaombeni mfanye mchakato wa bila upendeleo wowote ili niweze kupata mtoto yatima wa kike ambaye amefaulu mtihani lakini hana kabisa uwezo wa kusomeshwa sekondari".Aliongeza kuwa ukimgusa mtoto yatima ama mjane ni wazi unakuwa umemgusa Mwenyezi Mungu.

Mary alisema aliomba nafasi hiyo ili kuwatumikia wanawake wa mkoa wa Mbeya, katika kuwaletea maendeleo lakini hilo litafanikiwa iwapo nao watatoa ushirikiano wa dhati na kujenga umoja baina yao.

"Wanawake wa mkoa wa Mbeya na sisi umefika wakati tunatakiwa tuone wivu kwa wanawake wenzetu wa mikoa ya kaskazini ambao wanazidi kupiga hatua za kimaendeleo lakini sisi tunaendelea kupigana majungu na kutopendana" alisema Mary.

No comments:

Post a Comment