Sunday, July 19, 2009

MWANAMKE AJIUA KWA KUJIRUSHA KUTOKA GHOROFANI

MWANAMKE aliyekuwa ametoka kujifungua, Hellena Kambanga (29) amejiua baada ya kujirusha dirishani akiwa ghorofani ya tatu, hospitali ya Rufani Mbeya, kitengo cha Wazazi Meta, alikokuwa amelazwa.

Imeelezwa kuwa Hellena alijirusha kutoka wadi namba nne iliyopo ghorofani, saa 11:00 asubuhi, mara baada ya kumalizia dripu ya damu aliyokuwa ameongezewa mwilini baada kuishiwa wakati wa kujifungua.

Akithibitisha tukio hilo jana, mdogo wa marehemu ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha IFM Dar es Salaam, akiwa mwaka wa pili aliyejitambulisha kwa jina la Shida Kambanga, alisema marehemu ameacha mtoto huyo ambaye ana umri wa wiki mbili sasa.

Shida alikuwa akitoa maelezo hayo kwa kushirikiana na mdogo wake alijitambulisha kuwa anaitwa Amina.

Shida alisema hiyo ilikuwa ni mimba ya pili, kwa dada yake huyo ambaye alikuwa anaishi eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam na mumewe, na alikuwa amekuja mkoani Mbeya ambako ndipo alipozaliwa kusalimia ndugu na jamaa.

“Alikuwa anaumwa homa za mara kwa mara ambazo ni za kawaida kwa mwanamke mjamzito…siku za kujifungua zilipotimia alifanikiwa kujifungua salama kitengo cha Wazazi Meta, lakini alikuwa amepungukiwa damu mwilini” alisema Shida.

Aliongeza kuwa mara baada ya kuongezewa damu, marehemu Hellena alikuwa anaendelea vizuri na siku moja baada ya kumaliza dripu ya mwisho ya damu aliyokuwa amewekewa ndio aliamua kujirusha kutoka dirisha.

Kwa mujibu wa mdogo huyo wa marehemu, inaonyesha kuwa Hellena hakuwa na uangalizi wowote kutoka kwa wauguzi wa zamu siku hiyo hali iliyopelekea aweze kuamka muda huo wa alfajiri, kupanda dirishani na kujirusha hadi chini.

Alifafanua kuwa kutokana na utaratibu uliopo kitengo hicho cha Wazazi Meta, ndugu huwa hawaruhusiwi kulala na mgonjwa hivyo walipofika saa 12:00 asubuhi kumjulia hali ndipo walipopewa taarifa hizo.

Shida alisema:”Mara baada ya kujirusha kutoka juu ghorofani, dada alipata majeraha ya ndani kwa ndani mwilini na alikuwa akilalamika maumivu makali ya mgongo hali iliyopelekea ahamishiwe hospitali ya Rufani Mbeya kwa matibabu zaidi”.

Aliongeza kuwa Hellena alifariki dunia siku ya pili tangu afikishwe hospitalini hapo, na tayari amezikwa katika makaburi ya Mianzini yaliyopo eneo la Nzovwe jijini Mbeya, ambapo mtoto wake mchanga amechukuliwa na mama yao kwenda kulelewa Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi wa hospitali ya Rufani Mbeya, Dk. Eliuter Samky alipofuatwa ili kutoa ufafanuzi kuhusiana na tukio hilo, alisema hana taarifa zozote hivyo hawezi kuliongelea suala hilo.

“Mimi sina taarifa kuhusu kutokea kwa tukio hilo, hivyo siwezi kutoa maelezo yoyote…ningekuwa nimepewa taarifa ningesema, kifupi hakuna tukio kama hilo hospitalini hapa” alisema Dk.Samky.

No comments:

Post a Comment