Sunday, July 19, 2009

JAJI MKUU WA TANZANIA ALONGA KUHUSU WATUHUMIWA WA UFISADI.

JAJI Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhan, amesema mahakama haiwatambui watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi kuwa mafisadi hadi pale ushahidi dhidi yao utakapopelekwa na kutiwa hatiani.

Alisema ni vyema wananchi wote wenye ushahidi unaoweza kuwatia hatiani watuhumiwa hao waupeleke mahakamani ili kesi hizo ziweze kukamilishwa lakini siyo kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuilazimisha kuwatia hatiani.

“Tuleteeni ushahidi ili tuweze kuufanya kazi lakini hadi sasa hawa sisi mahakama tunawatambua kuwa ni watuhumiwa lakini siyo mafisadi…tukiruhusu kuingiliwa ni wazi uhuru wa mahakama utakuwa unachezewa” alisema Jaji Mkuu Ramadhan.

Jaji Mkuu Ramadhan ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, aliyasema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Mahakama wa wilaya zote na wale wa mkoa wa Mbeya, katika ukumbi wa Dk.Ali Shein.

Alisema umma unatakiwa usiiigilie mahakama katika utendaji wake wa kazi na kutoa mfano kuwa hata Yesu (Nabii Issa), alipopelekwa kwa Pilato ili amtie hatiani, Pilato alinawa mikono baada ya kuona kuwa mtu huyo hana hatia hivyo hawezi kumuhukumu kwa kuwa tu wayahudi wanataka ahukumiwe.

“Mfano huu ni mojawapo ya hofu ya uhuru wa mahakama unavyoweza kuingiliwa…na ndiyo maana Pilato alinawa mikono kuonyesha kuwa mahakama imemuona hana hatia hivyo haiwezi kumuhukumu pasipo kuwa na ushahidi” alisema Ramadhan.

Aliongeza kuwa hisia ya uhuru wa mahakama siyo ndio itamfanya Jaji Mkuu ashindwe kukaa na Rais Jakaya Kikwete, Waziri ama mkuu wa mkoa kwa madai atashindwa kufanya kazi yake ipasavyo.

Alisema:”Jaji Mkuu hawezi kumuingilia na kumuambia Jaji yeyote kuhusu nini cha kufanya kwa kesi iliyopo mbele yake, kwani Jaji ndie mwenye jukumu la kuiendesha kesi hiyo hivyo huwezi kumshika na vivyo hivyo umma nao unatakiwa usiingilie uhuru wa mahakama”.

Aidha, Jaji Mkuu Ramadhan alisema amekuwa anapokea barua nyingi kutoka kwa wabunge na wakuu wa wilaya nchini zikimtaka awahamishe mahakimu kutoka maeneo yao kwa kutuhumiwa kutowajibika katika utendaji wao wa kazi huku wengine wakituhumiwa kwa vitendo vya kupokea rushwa.

Alisema dawa ya tatizo hilo ipo mikononi wa Mtume hizo za Mahakama ambazo kazi yake kubwa ni kuhakikisha kuwa mahakimu wanakuwa na nidhamu na wanafanya kazi zao kwa kufuata misingi ya sheria iliyopo na siyo nje ya hapo.

Aliongeza kuwa kumhamisha hakimu kutoka sehemu moja kwenda nyingine siyo suluhisho, bali kinachotakiwa ni Kamati hizo kukutana mara kwa mara ili kuyafanyia kazi malalamiko wanayokuwa nayo kuhusu mahakimu katika maeneo yao.

Jaji Mkuu alisema:”Juhudi za Tume ni kushughulikia pia maslahi ya watumishi wote wa mahakama…ukiacha nidhamu kwa majaji na mahakimu, lakini pia kuna madhambi mengi yanafanywa na makarani pamoja na wahudumu wa mahakama zetu”.

No comments:

Post a Comment