Thursday, July 23, 2009

WANAWAKEW WATAKIWA KUJITOKEZA KUWANIA UONGOZI SERIKALI ZA MITAA

WANAWAKE mkoani Mbeya, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa, kupitia Chama Cha Mapinduzi, kwani uwezo wa kuongoza wanao.

Imeelezwa kuwa kitu kinachowakwamisha wanawake kushinda nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi ni tabia ya kuonea wivu na kupigana majungu na kutosaidiana.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Mwanjelwa, katika ziara zake za kutembelea wilaya zote za mkoa wa Mbeya kuwashukuru wanawake kwa kumchagua katika nafasi hiyo na pia kuangalia uhai wa jumuia na CCM kwa jumla.

Mary alisema umefika wakati wanawake wanatakiwa kujiamini kuwa wanaweza na kwa kufanya hivyo ni wazi hawataweza kushindwa kushinda katika nafasi mbalimbali watakazoomba kuwania kupitia Chama Cha Mapinduzi.

"Tujenge mahusiano mazuri baina yetu sisi wanawake ili tuweze kuasonga mbele, kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi...tupo katika nafasi hizi kwa nia ya kukitumikia Chama na siyo nje ya hapo" alisema Mwanjelwa.

Aliongeza kuwa itakuwa sifa kubwa kwa CCM na wanawake mkoani hapa, iwapo wanawake wengi watashinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao wa serikali za Mitaa.

Alisema, jumuia ya UWT mkoani hapa imekuwa inalegalega kutokana na wanawake kuendekeza majungu na kutopendana kwa sababu zisizokuwa za msingi hali ambayo haikijengi Chama bali inakibomoa.

Mjumbe huyo wa Baraza la UWT TAifa, alisema umefika wakati wanawake mkoani hapa na Tanzania kwa jumla kuachana na wale wanaowaona kuwa wamekuwa wanawachonganisha na kuendeleza majungu ndani ya jumuia na CCM Kwa jumla ili kukifanya Chama kizidi kuimarika na kukubalika kwa wananchi wengi.

Naye Katibu wa UWT mkoa wa Mbeya, Mwanaidy Mbisha, alisema uhai wa Chama na jumuia zake utaonekana pale wanawake watakapokuwa wanalipia kadi zao kwa wakati, kuingiza wanachama wengi na pia kuhakikisha kuwa wanavaa sare za Chama katika shughuli zozote za Chama.

Mwanaidy alisema pia wanawatakiwa kuhakikisha wanafanya vikao vya mara kwa mara kwa mujibu wa Katiba na kunapokuwa na tofauti baina yao basi ni vyema watumie vikao halali vya Chama kumaliza tofauti zao kwa maslahi ya CCM.

"Hamfanyi vikao vya jumuia katika ngazi zenu za matawi na kata...lakini nafikiri tatizo kubwa malokuwa nalo ni kudhani kuwa hamna ajenda za kuitisha vikao hivyo.Lakini hata suala la kuhamasisha kulipia kadi nalo mnaweza kulifanya kuwa ajenda ya kikao chenu" alisema Mwanaidy.

Katika ziara hiyo Mary amekuwa akitoa msaada wa shati za CCM, kwa wajumbe wa Baraza la UWT wa wilaya na kadi mia moja za UWT ili kuziwezesha ofisi za UWT Katika wilaya husika ziweze kutunisha mfuko na kuingiza wanawachama wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment