Wednesday, May 20, 2009

BOB MARLEY ATIMIZA MIAKA 28 TANGU KUFARIKI DUNIA

MFALME wa muziki wa Reggae duniani, marehemu Robert Nesta Marley, maarufu zaidi Bob Marley, alizaliwa Februali 6,mwaka 1945, katika eneo liitwalo Nine Miles,lililopo kitongoji cha Mtakatifu Ann, nchini Jamaica.

Akiwa bado kijana mdogo,Bob Marley alianza kuimba nyimbo akishirikiana na marafiki zake Bunny Livingston and Peter Mackintosh, na vijana hao hatimaye wakaunda bendi yao iliyoitwa The Wailing Wailers. Kundi hilo lilifanikiwa kutoa nyimbo chache zilizopata umaarufu kabla ya kusambaratika mnamo mwaka 1966.Vijana hawa watatu pia walijiingiza katika imani ya Rastafarianism, dini ya amani ambayo waumini wake wanaamini kuwa aliyekuwa mfalme wa Ethiopia, marehemu Haile Selassie, atawaongoza watu weusi kwenda katika nchi yao ya asili.

Mnamo mwaka 1966, Bob Marley alimuoa muimbaji, Rita Anderson. Siku moja baada ya ndoa yake, Marley aliondoka Jamaica na kuelekea nchini Marekani ambapo alipata kazi ya kuwa dereva.Mwezi wa Novemba mwaka huo huo, alirejea nchini Jamaica na kwa kushirikiana na Rita, walianza kutengeneza duka la kuuza kanda za muziki.

Bob Marley pia aliungana na Livingston and Tosh (Mackintosh), na kwa pamoja waliunda kundi lao jipya lililoitwa The Wailers. Mwaka 1970, Aston Barrett (mpiga gitaa la besi) na kaka yake Carlton Barrett (mpiga dram), walijunga na bendi hiyo.
Aina yao ya kipekee ya muziki wao, ilivuma sana nchini Jamaica na mnamo mwaka 1972, bendi ya The Wailer iliingia mktaba na kampuni ya Island Records, iliyoanzishwa na mzungu aliyekuwa na asili aliyejulikana kwa jina la Chris Blackwell.

Mwaka uliofuata The Wailers waliachia albamu yao ya kwanza "Catch A Fire", iliyokuwa na vibao moto kama "Stir it Up" na "Stop That Train", na walienda ziara ya Uingereza na Marekani kuitangaza albamu yao.Wakiwa Marekani nchini bendi hiyo ilipiga pamoja na bendi ya mwanamuziki Bruce Springsteen, katika ukumbi wa Max's Kansas, uliopo jijijini New York.
Mwezi wa Novemba mwaka 1973, The Wailers, waliachia albamu yao ya pili iliyoitwa "Burnin". Miongoni mwa nyimbo maarufu ya "I Shot the Sheriff" ambayo Eric Clapton aliuchukua na kuipandisha hadi kushika namba moja katika chati mnamo mwaka 1974.
Baada ya albamu hiyo ya Burnin, Tosh na mwenzake Livingston waliondoka katika bendi ya The Wailers na kila mmoja kuamua kupiga muziki kama mwanamuziki wa kujitegemea.

Sasa kuanzia hapo ndio bendi hiyo ilipoanza kujulikana kama Bob Marley and The Wailers. Mwaka huo huo waliipua albamu yao iliyoitwa "Natty Dread" , ikiwa nyimbo moto moto zilizojipati umaarufu mkubwa kama "Lively Up Yourself" na "No Woman No Cry". Waitikiaji katika albamu hiyo ni kinadada watatu walijulikana zaidi kama I-Threes.

Waitikiaji hao mbali ya mke wake Rita, pia walikuwemo Judy Mowatt na Marcia Griffiths. Pia katika albamu hiyo walishiriki wanamuziki wawili wapya ambao ni Al Anderson (mpiga gitaa) na Bernard 'Touter' Harvey aliyekuw akipiga Kinanda (keyboards).
Mwaka 1976, albamu iliyopewa jina la "Rastaman Vibration",ilitolewa na ilikwenda na kuchukua nafasi ya nane katika chati ya muziki. Kikiwemo kibao maridhawa cha "Roots, Rock, Reggae".

Baadaye mwaka huo huo mnamo Desemba 3, Marley na mkewe Rita walipigwa risasi na baada ya kuvamiwa nyumbani kwao na kundi kubwa la watu wenye silaha ambao ilidaiwa kuwa walikuwa wakitokea chama Cha Labor nchini Jamaica.

Shambulio hilo lilikuwa na nia ya kumzuia Marley kufanya tamasha lililomuhusisha Waziri Mkuu Michael Manley. Baada ya kupatiwa matibabu hospitalini, Marley alijificha katika eneo liitwalo Jamaica's Blue Mountains hadi siku ya tamasha, baadaye yeye pamoja na mkewe waliondoka nchini Jamaica na kuishi nje ya nchi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.
.
Baada ya kuondoka Jamaica, wanandoa hao walihamishia makazi yao jijini London, nchini Uingereza ambako Bob Marley alirekodi albamu iitwayo "Exodus".Albamu hii iliingia sokoni mwaka 1977, ikiwa na nyimbo "Waiting in Vain" na "Jamming".

Ni mwaka huo huo ambapo madaktari waliugundua ugonjwa wa Kansa katika kidole cha Bob Marley. Walimshauri awaruhusu wakikate kidole hicho ili kuiondoa kabisa Kansa lakini Marley alikataa upasuaji huo kwa sababu ulikuwa ni kinyume na imani yake ya Rastafarian.

Maisha yakazidi kusonga mbele, ambapo mwaka 1978, bendi ya The Wailers walitoa albamu ya "Kaya", iliyokuwa na vibao matata kikiwemo kijulikanacho kwa jina la "Is This Love".

Wakiwa katika ziara ya kuitangaza albamu yao hiyo, walitumbiza katika ukumbi maarufu wa Madison Square, uliopo jijini New York, na onyesho hilo lilirushwa moja kwa moja hewani na kupatikana albamu nyingine iliyopewa jina la "Babylon By Bus". Ilifuatia albamu nyingine iliyoitwa "Survivor", mnamo mwaka 1979.
"Uprising" ni albamu ya mwisho kutolewa na Bob Marley katika kipindi cha maisha yake alichoishi hapa duniani.na bendi ya The Wailers walipanga kufanya onyesho la pamoja na kundi maarufu la Commodores katika ukumbi wa Madison Square Garden.

Akiwa New York, Marley alianguka akiwa anafanya mazoezi katika viwanja vya Central Park. Ikaja kubainika kuwa Kansa ilikuwa imesambaa kwenye mapafu na ubongo na hatimaye mfalme huyu wa Reggae asiye na mbadala wake alifariki dunia.

Bob Marley alifariki Mei 11,mwaka 1981, akiwa na umri mdogo wa miaka 36 tu katika hospitali ya Miami ambapo mazishi yake yalifanyika nchini Jamaica na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 100,000.

Mwili wake uliwekwa katika jumba la makumbusho lililopo katika mji aliozaliwa wa Nine Miles nchini Jamaica.Na katika kutambua mchango wa Bob Marley, kila ifikapo siku yake ya kuzaliwa yaani Februali 6, siku hiyo imewekwa kuwa ni mapumziko nchini Jamaica.

Mnamo mwaka 1992, albamu maarufu ya iitwayo "Songs Of Freedom", ilitolewa ikiwa na nyimbo zake kuanzia ile ya kwanza iliyotolewa mwaka 1962 ya "Judge Not" hadi zile za mwaka 1980 zikiwemo "Redemption Song".

Huyu ndiye Bob Marley ambaye pamoja na kufariki miaka mingi iliyopita miaka 28, iliyopita lakini muziki wake bado haujachuja kwani nyimbo zake zina ujumbe mzito ambao utadumu daima milele na milele.

00000

No comments:

Post a Comment