Tuesday, May 26, 2009

TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAPONDA HUKUMU...

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imesema kuwa kuachiwa huru kwa watuhumiwa watatu, raia wenye asili ya kiasia waliokuwa wanatuhumiwa kwa mauaji ya mwanafunzi Swaibu Omary, kumegubikwa na harufu ya rushwa.

Kamishna wa Tume hiyo, Bernadeta Gambishi, aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Mwanjelwa, jijini Mbeya kuelezea kazi ya Tume hiyo kwa wananchi.Alikuwa akijibu swali la mmoja wa wananchiu aliyetaka kujua Tume hiyo ina mtazamo gani kuhusu hukumu hiyo.

Tume hiyo ipo mkoani hapa akitokea mkoa jirani wa Iringa, kwa ajili ya kukagua hali za magereza nchini baada ya kufanya ziara mnamo mwaka 2006/07, hivyo inatembelea tena kuona kama kile walishoishauri serikali kuhusu hali za magereza kimetekelezwa.

"Haiwezekani watuhumiwa hao watatu waachiwe baada ya kusota jela kwa muda wa mwezi mmoja...kuachiwa huku kunaonyesha kuna mazingira makubwa ya rushwa.Tukifanikiwa kukutana na ndugu wa marehemu tutawashauri ili wakate rufaa kwa ajili ya kufungua upya kesi hii ili haki itendeke" alisema Bernadeta.

Watuhumiwa hao ndugu kutoka familia moja ni Samir Muzrai, Faizy Abdulrasul na Hassan Abdul.

Kuachiwa kwa wapakistani hao kwa kipindi kifupi ambao walikamatwa April 6, mwaka huu kumezua maswali mengi kutoka kwa wananchi wa wilaya ya Mbarali ambao wanahoji kwa nini kesi nyingine za mauji watuhumiwa wamekuwa wakiwekwa mahabusu kwa muda mrefu wa zaidi ya miaka miwili bila kesi zao kuanza kusikilizwa.

Wananchi wamelitupia lawama jeshi la polisi mkoani hapa, kuwa linajenga matabaka katika kupeleleza kesi za mauaji kutokana na watu wenye kipato kikubwa upelelezi wao kufanyika haraka huku maskini wakisota kwa muda mrefu mahabusu.

Naye Wakili wa Serikali Mkoa wa Mbeya, Ayoub Mwenda, akizungumza na waandishi wa habari, alithibitisha kuachiwa hutu kwa watuhumiwa hao baada ya ofisi yake kujiridhisha na maelezo ya upelelezi uliofanywa na polisi pamoja na vipimo vya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu.

Mwenda alisema kwa mujibu wa upelelezi uliofanywa na polisi kutokana na tukio hilo ni kwamba mwanafunzi huyo alifariki dunia kwa kuumia baada ya kuruka kutoka juu ya gari na hivyo kusababisha kuumia vibaya kichwani.

Aliongeza kuwa daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu alieleza kuwa mwanafunzi huyo alifariki kwa kuumia na siyo kwa kipigo kama ilivyodaiwa awali hivyo kutokana na maelezo ya polisi na daktari, serikali imeamua kuwafutia shitaka baada ya kubaini kuwa watuhumiwa hawakuhusika na mauji ya mwanafunzi huyo.

"Pamoja na watuhumiwa hao kuachiwa huru iwapo watajitokeza watu wengine wakatoa ushahidi wa kudhibitisha kuwa raia hao wa Pakistani walimuua mwanafunzi huyo watuhumiwa hao wanaweza wakakamatwa tena na shauri lao likaanza kupitiwa upya" alisema Mwenda.

Kwa upande wake Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mbarali, Mustaphir Siyani, alisema watuhimiwa hao wameachiwa huru Mei 18 mwaka huu baada ya kubainika kuwa hakuna ushahidi wa kutosha wa kesi hiyo kutokana na upelelezi uliofanywa na polisi na kuupeleka kwa wakili wa serikali.

Alisema hata hivyo iwapo kutapatikana ushahidi wa kutosha jamuhuri ina uwezo wa kuwakamata watuhumiwa na kuwafunguliwa upya shitaka kutokana na kifungu cha 91 cha sheria ya makosa ya mauaji.

Awali jeshi la polisi Mkoani Mbeya lilieleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa kutuhumiwa kuumua mwanafunzi wa shule ya sekondari ya mkoani Kigoma baada ya kumkuta akiiba matunda aina ya mapera shambani mwao April 6 mwaka huu.

0000

No comments:

Post a Comment