Saturday, May 30, 2009

MHANDISI MSHAURI WA MAJENGO MKOA WA MBEYA AMCHEFUA RC.

MKUU wa mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, amemuagiza Katibu Tawala, Beatha Swai, kumuondoa Mhandisi mshauri wa majengo, Aidan Ngwada, kufuatia kuboronga katika utendaji wake wa kazi.

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia malalamiko mengi kutolewa kuhusu idara ya Uhandisi mkoani hapa, hali inayopelekea miradi mingi inayofanyika kuwa chini ya kiwango cha ubora.

Mwakipesile alifikia hatua hiyo jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa (RCC), kilichofanyika jana katika ukumbi wa Dk.Ali Shein, baada ya wakuu wa wilaya watatu, kumnyoshea kidole Ngwada, kuwa kazi anazosimamia hazina kiwango.

Alisema kuwa idara hiyo ni mbovu ambapo fedha nyingi zinazotolewa na serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali zimekuwa zinatumika isivyo huku miradi hiyo ikiwa haina ubora wowote.

"Tumechoka na kazi mbovu za Uandisi katika serikali ya mkoa wa Mbeya na hatuwezi kuendelea kukaa kimya wakatri fedha za serikali zinatumika vibaya huku miradi ikiwa haina ubora unaotakiwa" alisema Mwakipesile.

Aliongeza kuwa hataki kuwa sehemu ya wizi huo unaofanyika katika idara hiyo na awali alishawahi kumtaka aliyekuwa Katibu Tawala mkoani hapa Assumpta Ndimbo, kumuondoa Mhandisi huyo lakini haelewi ni vipi anaendelea kushikilia wadhifa huo hadi leo.

Mkuu wa mkoa alisema:"Sitaki kuwa sehemu ya wizi huu, inawezekana wewe ni injinia mbovu, huna cheti na iwapo hivi vyote unavyo basi ni wazi unashirikiana na wengine katika wizi".

Alisema kuwa serikali imeajiri wahandisi kwa kila wilaya, lakini wamekuwa wanalipwa tu mishahara bila ya kufanya kazi zozote kutokana na ukiritimba unaofanywa na Ngwada wa kwenda kufanya kazi hizo badala ya kuziachia wilaya husika.

Akizungumza kwa hasira, Mwakipesile alisema hawezi kukubali yeye aonekane ni sehemu ya ubovu katika mkoa wa Mbeya, kwani kila siku amekuwa akipokea malamiko ya ujenzi mbovu wa barabara hasi nyumba za wakuu wa wilaya na makatibu Tawala wa wilaya.

"Hivyo nawaomba wajumbe tusiendelee kuchangia katika hili, kwani kwa kuwa Katibu Tawala Beatha yupo, amesikia na atalifanyia kazi...tumuachie hili mikononi mwake" alisema Mwakipesile.

Kufuatia hali ya hewa kuchafuka, mara baada ya Mkuu wa mkoa kumaliza kuitolea ufafabnuzi hoja hiyo iliyokuwa imeibuliwa na Wakuu wa wilaya za Chunya, Kyela na Mbeya, mnamo saa 7:20 mchana Ngwada alisimama na kutoka nje ya ukumbi na hakurejea tena hadi kikao hicho kinafungwa saa 9:00 alasiri.

Waandishi walipotoka nje ili kumuomba Ngwada atoe ufafanuzi kuhusu kilichotokea, aliwaomba wamuache kwani hajisikii vizuri na kuwa mapigo ya moyo (BP), hayapo salama.

No comments:

Post a Comment