Tuesday, May 26, 2009

MBUNGE MPESYA AMSHUKIA MKURUGENZI WA JIJI LA MBEYA.

MBUNGE wa jimbo la Mbeya mjini (CCM), Benson Mpesya, amesema kuwa maazimio yanayotolewa na baraza la madiwani yasiposimamiwa na kutekelezwa, anayepaswa kuwajibika ni Mkurugenzi na siyo vinginevyo.

Alisema kuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Mbeya,Elizabeth Munuo, ndiye anatakiwa awapange watendaji wake na kuwaelekeza kitu gani kinatakiwa kifanywe ndani ya jiji na siyo madiwani.

Mpesya aliyasema hayo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, waliotaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali, likiwemo suala la kukithiri kwa uchafu ndani ya jiji la Mbeya.

"Kazi ya madiwani ni kusimamia yale maazimio ili yatekelezwe...sasa maazimio yanapotolewa na baraza la madiwani yasipotekelezwa, mwenye matatizo hapo kwa mujibu wa kanuni na taratibu zetu ni yule anayetakiwa kuyasimamia maazimio" alisema Mpesya.

Aliongeza kuwa kazi ya madiwani ni kuamua, na kuadhimia kuwa kuanzia sasa wanataka takataka za mahali fulani ziondolewe, ama yanunuliwe magari kwa ajili ya kuzoa takataka, na mtekelezaji mkuu ni kiongozi wa kiserikali ambaye ni Mkurugenzi.

Mbunge huyo alisema hivyo ni vyema waandishi wa habari, wangekuwa wanahoji iwapo yale maazimo yanayoamuliwa na baraza la madiwani yanatekelezwa, ama la na ndipo wangejua ni nani wa kumkamata ili atoe ufafanuzi sahihi.

Mpesya alisema:"Na nyinyi ndugu zangu waandishi wa habari, ni figa la nne licha ya kuwa halipo ndani ya katiba...mimi ni miongoni mwa wabunge ambao nawakiri kabisa kuwa kazi yenu ya kuielimisha jamii ni nzuri".

Aliongeza kuwa hivyo waandishi wa habari wanatakiwa kujenga na kuwafanya viongozi wawe wamoja badala ya kuwabomoa, kwani wao ni figa halali lakini wakati mwingine hawaifanyi kazi hiyo kwani wanawasukuma mno wanasiasa katika kutekeleza majukumu.

Alisema ni vyema kukiwa na tatizo, basi kitafutwe kiini cha tatizo,na sityo kurusha rusha tu mambo bali wajue tatizo lipo wapi.

Katika hatua nyingine, Mpesya alithibitisha kuwa atakuwa ni mmoja wa wana-CCM watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo ya ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010.

Alisema zipo habari zinazoenezwa mitaani kuwa hatagombea ubunge mwakani, na aliwachekesha waandishi aliposema kuwa yeye atapata wapi nafasi ya kusema kuwa atatetea nafasi hiyo kama siyo kupitia vyombo vya habari.

"Na mimi natoa mapema azimio langu kuwa nitajitokeza tena katika uchaguzi mkuu ujao ili kutetea nafasi ya ubunge wa jimbo hili, hivyo wale wengine wenye nia nao wajipime ubavu...kwa kazi nilizozifanya katika kuteleleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ninao uhakika kuwa nitapata kura nyingi" alisema Mpesya.

No comments:

Post a Comment