ASASI isiyo ya kiserikali ya Maendeleo Trust Fund, iliyopo wilayani Kyela, inatarajia kuandaa siku maalumu ya Usiku wa Mwanamke wa Kinyakyusa, ili kusaidiana na serikali kuupiga vita ugonjwa wa Ukimwi.
Imeelezwa kuwa lengo la shughuli hiyo ni kupiga vita biashara ya ngono zembe ambayo imekuwa inachangia maambukizi mapya ya Ukimwi wilayani humo na mkoa wa Mbeya kwa jumla.
Mratibu mwezeshaji wa asasi hiyo, Amos Mwakabambo, alisema kuwa Usiku huo uliopewa jina la Mwanamke wa Kinyakyusa, utafanyika mapema mwezi Agost mwaka huu.
Mwakabambo aliongeza kuwa siku hiyo vikundi vya uzalishaji vya wanawake wajasiriamali na wanawake kwa jumla, vitapata fursa ya kuonyesha huduma wanazotoa na kuziuza pia kwa wananchi.
“Katika maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, wilaya ya Kyela ipo juu kitakwimu kwa mkoa wa Mbeya na taifa kwa jumla.Hivyo tukiwa kama jamii tunatakiwa kuonyesha jitihada zetu katika kukabiriana na janga hili” alisema Mwakabambo.
Aliongeza kuwa vile vile alisema kuwa wanataka kuibomoa dhana potofu ya kuwa biashara ya ngono ina soko la uhakika na inalipa tofauti na biashara nyingine.
Alifafanua usemi wake huo kuwa wapo baadhi ya wanawake wilayani humo, wanaojishughulisha na biashara ya ngono, ambao wanasema hawapo tayari kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali kama vile ushonaji.
Mwakabambo alisema:”Hawa huwa wanadai ya kwamba hawawezi kukaa na kupoteza muda wao kwa kuwasubiria wateja ambao hawana ahadi nao, wakati urithi wa bibi wanao na wameukalia tu”.
Mratibu huyo alisema kuwa Mei 11, mwaka huu watakutana na vikundi hivyo vya wanawake wajasiriamali, uongozi wa halmashauri ya wilaya Kyela na wadau mbalimbali ili kuunda Kamati ya Maandalizi ya shughuli hiyo.
Kuhusu zawadi alisema mshindi wa kwanza hadi wa tatu, watapewa zawadi ya shilingi 500, 000 kila mmoja ambapo pia kutakuwa na mashindano ya kuendesha baiskeli kwa wanawake watakaoshiriki shughuli hiyo.
Mwakabambo alisema katika mashindano ya baiskeli mshindi wa kwanza atazawadiwa baiskeli yenye thamani ya shilingi 150,000, wa pili atapata shilingi 50,000 wakati mshindi wa tatu atajinyakulia shilingi 30,000.
Aliongeza kuwa washindi wengine watakao kuwemo katika nafasi kumi bora, watapata kifuta jasho cha 10,000 kila mmoja pamoja na zawadi ya fulana maalumu zitakazokuwa zimeandaliwa kwa shughuli hiyo.
Ameyaomba makampuni binafsi kujitokeza kudhamini usiku huo wa kihistoria kwa wilaya ya Kyela ili kuweza kulitokomeza gonjwa la Ukimwi ndani ya wilaya hiyo na mkoa wa Mbeya kwa jumla.
0000000
Wednesday, May 20, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment