WIMBI la mauaji ya kinyama ya wanawake, katika eneo la Mabatini jijini Mbeya, linaelekea kuota mizizi, kufuatia mwanamke mwingine kuuawa kikatili kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.
Katika tukio hilo, wanawake wengine wawili ambao ni ndugu wa marehemu walijeruhiwa vibaya maeneo ya kichwani na wanaendelea kupata matibabu hospitali ya Rufani Mbeya.
Marehemu ametajwa kuwa ni Vena Kasokela (25), wakati waliojeruhiwa wakitajwa kuwa Emmy (46) na Lydia John (58).
Hivi karibuni mwanamke mjamzito, Jacquliene Mwasunga (18), aliuawa kikatili eneo hilo hilo huku mtoto wa dada ake, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili sekondari ya Legico, Upendo Mwasunga (16), akijeruhiwa kichwani na kukatwa sikio lake kushoto.
Akithibitisha kutokea kwa tukio la kinyama, Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Zelothe Stephen, alisema lilitokea juzi saa 12:00 asubuhi, baada ya watu wasiofahamika kuivamia nyumba hiyo.
Akifafanua, Stephen alisema kuwa marehemu Vena na majeruhi Emmy, walikuwa ni wageni waliokuwa wamefikia kwa mwenyeji wao Lydia ambaye ni mfanyabiashara wa pombe za kienyeji katika klabu moja iliyopo eneo hilo.
"Mara baada ya kuvamiwa, wanawake wote watatu walianza kupigwa maeneo ya kichwani na kitu kizito, na kusababisha majeraha ambapo wote walikimbizwa hospitali ya Rufani Mbeya kwa matibabu" alisema Stephen.
Aliongeza kuwa ilipofika saa 4:00 asubuhi, zilipatikana taarifa kuwa mmoja wa majeruhi, Vena Kasokela, amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu ili kuokoa maisha yake.
Stephen alisema:"Taarifa za awali kuhusu chanzo cha mauaji haya, zinaonyesha kuwa huenda tukio hili ni la ulipizaji kisasi, kwani majeruhi Emmy alikuwa ameolewa na ameachika hivi karibuni".
Alisema kuwa polisi wanachukulia mauaji hayo kama ni ya kulipiza kisasi, kwani watuhumiwa wa mauaji hao hawakuchukua kitu chochote kutoka nyumba hiyo, hali ambayo ingeashiria kuwa walikuwa ni majambazi wa kawaida.
Aliongeza kuwa kikosi cha upelelezi cha jeshi hilo, kimepelekwa eneo la Mabatini kwa ajili ya kuendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo la kinyama.
Alisema hivyo polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio yote mawili,aliyoyata kuwa ni kujeruhi na mauaji kwani wana uhakika kuwa wakifanikiwa kuwakamata watuhumiwa basi ni wazi ndio watakuwa wameshiriki katika matukio yote mawili.
Lakini wananchi wa eneo la Mabatini waliozungumza na gazeti hili, kwa nyakati tofauti, wamelitupia lawama jeshi la polisi mkoa kwani hadi leo halijafanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wa mauaji ya mwanamke mjamzito, Jacquliene.
Waliongeza kuwa hali ya usalama iliyopo hivi sasa maeneo hayo, hasa kwa wanawake inawatia hofu kwani matukio yote mawili ya mauaji hayo ya mfululizo, yamekuwa yakitokea saa za asubuhi.
"Tunaomba jeshi la polisi lifanye kazi zake kwa ufanisi ili kuweza kuwatia mbaroni watuhumiwa hawa wa mauaji yanayotokea mfululizo... kwa kweli hivi sasa tunaishi kwa maashaka hatujui kesho itakuwa zamu ya nani" walisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment