Friday, May 29, 2009

TANROADS MBEYA WAWEKWA KITI MOTO.

WAJUMBE wa kikao cha Bodi ya barabara mkoa wa Mbeya, wamemuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),mkoa kuhakikisha kuwa bajeti ya barabara inayotakiwa kupitishwa inapitiwa kwanza na kikao hicho.

Imeelezwa kuwa TANROADS wamekuwa wanapitisha bajeti hiyo na kuamua wao barabara za kuzitengeneza badala ya zile zinazotakiwa na wananchi wa wilaya husika.

Wakichangia katika kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika jana.chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa mkoa wa Mbeya,wajumbe hao walisema kuwa barabara zinazotengenezwa na TANROADS zinatakiwa kujibu kero za wananchi na siyo nje ya hapo.

Walisema kuwa hivyo kuanzia bajeti ijayo ni lazima kabla ya kupitishwa iwe inaletwa kwenye kikao hicho kujadiriwa ili barabara zitakazotengenezwa ziwe ni zile zinazopewa kipaumbele na wananchi na siyo wakala huyo wa barabara.

“Ni vyema hili lifanyiwe kazi ili barabara zile zinazotakiwa na wananchi kutokana na umuhimu wake ndizo zipewe kipaumbele cha kwanza na siyo zile ambazo TANROADS mmekuwa mnaziamua na kuzipangia bajeti bila ya kutushirikisha” walisema.

Waliongeza kuwa mabadiliko hayo yasipofanyika ni wazi hadi tunaingia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,barabara nyingi zitakuwa zimetengenezwa lakini zitakuwa hazijibu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005-2010.

Walisema haiwezekani TANROADS wawe wanaamua barabara zipi za kutengenezwa, kupanga bajeti na kisha kuileta kwenye kikao cha Bodi ya Barabara kwa ajili ya kuwasomea tu wajumbe,hali ambayo inakuwa haisadii.

“Tuachane na utaratibu huu uliopo hivi sasa kwani barabara hizi ni zetu na nyie TANROADS ni wakala tu wa kuzisimamia….kwani wananchi ndio wanaoamua barabara ipi itengenezwe kutokana na umuhimu wake na siyo nyie ndio muwe mnawaamulia” walisema.

Kufuatia hali hiyo,Mkuu wa mkoa Mwakipesile alikubaliana na hoja hizo za wajumbe na kuwa kuanzia sasa bajeti hiyo iwe inaletwa kwenye kikao hicho,kujadiriwa kabla ya kuanza kutekelezwa ili barabara zenye umuhimu kwa wananchi ndizo zipewe kipaumbele kikubwa cha kutengenezwa.

No comments:

Post a Comment