Wednesday, May 20, 2009

PROFESA MWAKYUSA AWAPA SOMO WAGANGA WAKUU WA MIKOA.

WAZIRI wa afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya nchini, kupiga vita tabia ya watoa huduma wachache miongoni mwao wenye lugha chafu, ubaguzi, ukatili unyanyapaa na dharau.

Sambamba na hilo amewataka kuendeleza juhudi katika kupambana na adui rushwa sehemu zao za kazi ili kuongeza imani zaidi ya wananchi katika vyombo vyao vya huduma.

Waziri Mwakyusa aliyasema hayo hivi karibuni wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Waganga Wakuu wa mikoa na Wilaya uliofanyika katika ukumbi wa Bebjamini Mkapa jijini Mbeya.

Alisema kuwa tabia hizo mbaya ni lazima zikemewe kwa nguvu zote kwani zinawatia doa na kuwachafua watumishi waadilifu ambao ndiyo wengi.

Profesa Mwakyusa aliongeza kuwa anatambua kuwa wanafanya kazi zao katika mazingira magumu lakini pamoja na hayo wameendelea na kazi za kutibu, kukinga, kutoa ushauri na kuwafuata wagonjwa na wateja wao hadi vijijini na majumbani mwao.

“Ninawaomba wote muendelee kufanya kazi nzuri, kuongeza juhudi na upendo na pia kuwa na tabia ya kuwajali na kuwaruhumia wagonjwa kwa mateso wanayoyapata kila siku” alisema Profesa Mwakyusa.

00000

No comments:

Post a Comment